• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China yaweka vipaumbele vya kazi kwenye mageuzi ya mfumo wa matibabu katika nusu ya pili ya mwaka

    (GMT+08:00) 2020-07-28 19:09:46

    Ofisi Kuu ya Baraza la Serikali la China hivi karibuni imetangaza vipaumbele vya kazi kwenye kuimarisha mageuzi ya mfumo wa huduma za afya katika nusu ya pili ya mwaka huu, kwa lengo la kuendelea kutafuta utatuzi wa suala la ugumu na gharama kubwa za huduma za matibabu.

    Katika miaka ya hivi karibuni, mageuzi ya mfumo wa huduma za afya yamekuwa ni jambo linalofuatiliwa sana kwenye jamii. Akiongea kwenye mkutano na wanahabari kuhusu sera za Baraza la serikali uliofanyika leo, naibu mkurugenzi wa Kamisheni ya Afya ya Taifa ya China Bw. Wang Hesheng, amesema vipaumbele vya kazi katika nusu ya pili ya mwaka kwenye kuimarisha mageuzi ya mfumo wa matibabu vilivyotolewa hivi karibuni na Baraza la serikali la China, vimezingatia zaidi huduma za kinga dhidi ya magonjwa, na kuendelea na juhudi za kutafuta utatuzi wa suala la ugumu na gharama kubwa za huduma za afya, ili kutoa uungaji mkono imara katika kuhakikisha usalama wa maisha na afya ya wananchi. Anasema,

    "Kwanza ni kuimarisha ujenzi wa mfumo wa afya ya umma, kupitia kukamilisha mfumo wa kinga na udhibiti wa magonjwa, mfumo wa usimamizi na kutoa tahadhari kuhusu magonjwa ya kuambukiza, na mfumo wa ugavi wa vifaa vya dharura vya afya ya umma, kufanya vizuri kazi ya kuzuia na kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona katika majira ya mpukutiko na majira ya baridi, na kuimarisha ujenzi wa vikosi kazi vya afya ya umma. Pili ni kuimarisha utekelezaji wa Harakati ya Afya China, ikiwemo kuendelea kuboresha mazingira ya maisha na ya kazi, kuelimisha umma kuwa na mienendo mizuri ya maisha, kuimarisha huduma za afya kwa makundi maalumu ya watu, kuinua kiwango cha kinga na tiba ya magonjwa sugu, na kuongeza nguvu katika kinga na udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza, magonjwa ya kieneo na kikazi. Tatu ni kuimarisha mageuzi kwa hospitali za umma. Nne ni kuimarisha mageuzi kwa mfumo wa bima ya matibabu. Tano ni kukamilisha mfumo wa ugavi wa dawa."

    Hivi sasa kutokana na juhudi za pamoja za serikali na wananchi, hali ya kinga na udhibiti wa ugonjwa wa virusi vya Corona nchini China imekuwa na mwelekeo mzuri, lakini mlipuko wa virusi hivyo pia umefichua dosari na matatizo yaliyopo kwenye mfumo wa huduma za afya nchini China. Akizungumizia suala hilo, Bw. Wang Hesheng amesema katika siku zijazo China itaimarisha uhakikisho katika nyanja tatu. Kwanza ni kukamilisha uhakikisho wa huduma za tiba wakati wa milipuko mikubwa ya magonjwa, na China itaunga mkono kila mkoa kujenga au kufanyia maboresho vituo kimoja hadi vitatu vya mwitikio kwa milipuko ya magonjwa.

    Pili ni kukamilisha uhakikisho wa ugavi wa vifaa tiba vya dharura, na kuzitaka taasisi za huduma za afya ziweke akiba ya kutosha ya vifaa tiba ikiwemo barakoa na nguo za kujikinga, ili kuweza kukabiliana na wimbi la kwanza la maambukizi.

    Tatu ni kukamilisha uhakikisho wa mipango ya matumizi ya miundombinu ya dharura ya kiafya, zikiwemo hospitali zinazohamishika na hospitali zilizoteuliwa kukabiliana na milipuko ya magonjwa.

    Ofisa huyo pia amesema, mwaka huu serikali kuu imeongeza maradufu uwekezaji katika miradi mbalimbali ya afya ya umma.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako