• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • RAGA: Kenya Harlequins Wajinyakulia Huduma Za Wanaraga Wawili Wa Kimataifa Kutoka Homeboyz RFC

    (GMT+08:00) 2020-11-04 17:09:34

    Kenya Harlequins wameimarisha kikosi chao kwa minajili ya kampeni za msimu ujao katika raga ya Kenya Cup kwa kujinasia huduma za wachezaji wawili wa kimataifa Joshua Chisanga na Emmanuel Mavala kutoka Homeboyz RFC. Chisanga na Mavala walijiunga upya na Homeboyz msimu uliopita baada ya kuwa nje kwa mwaka mmoja wakichezea RC Orkan Sochaczew ya Poland. Mwenyekiti wa Quins, Michael Wanjala amesema kwamba ujio wa wanaraga hao wawili kambini mwao utaimarisha zaidi kikosi chao na kuinua uthabiti wa kikosi kilichokosa fursa ya kufuzu kwa hatua ya mwondoano mnamo 2019. Quins walikamilisha kampeni za mwaka wa 2019-20 katika nafasi ya tisa baada ya kujizolea jumla ya alama 28 ambapo walisajili ushindi mara tano na kupoteza jumla ya michuano 11. Chisanga na Mavala wanajiunga na mwanaraga mwingine wa zamani wa Homeboyz, Mark Wandetto aliyeingia katika sajili rasmi ya Quins mnamo Mei 2020. Wandetto alikuwa miongoni mwa wanaraga tegemeo katika timu ya taifa ya Shujaa chini ya kocha wa zamani wa kikosi hicho, Paul Murunga. Alikuwa mchezaji wa pili baada ya Leroy Mbugua kutoka Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta kusajiliwa na Quins muhula huu. Wandetto alikuwa mhimili wa Homeboyz kwa misimu miwili iliyopita. Wanjala pia amefichua kwamba wanalenga kukamilisha usajili wa mchezaji Philip Ikambili kutoka Homeboyz na wanaraga wengine wawili wa USIU-A. Licha ya kwamba serikali bado haijaidhinisha kurejeshwa kwa michezo ya kugusana katika mojawapo ya hatua za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona, Quins wamekuwa wakijiandaa kwa msimu ujao wa 2010-21.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako