• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Mpango wa China kuvutia Wataalam, Tanzania tuanze kuthamini wa kwetu

  (GMT+08:00) 2016-11-15 10:04:50

  SIKU chache zilizopita nilibahatia kuhudhuria mkutano kati ya Waziri Mkuu wa China, Li Keqiang na wataalamu kutoka nje wanaofanya kazi hapa China.

  Kwenye mkutano huo unaofanyika kila mwisho wa mwezi Septemba kabla ya siku ya taifa ya China ambayo ni Oktoba 1, mbali na baadhi ya wataalamu kupewa tuzo maalum ya kutambua mchango wao, Waziri Mkuu wa China pia hujumuika na wataalamu hao na kubadilishana nao maoni kuhusu mambo yanayohusu sekta zao, mazingira yao ya kazi, maisha yao hapa China na hata maendeleo ya China kwa ujumla na changamoto zake.

  Utaratibu wa kutumia wataalamu wageni kuhimiza maendeleo ya nchi, ni moja ya njia zinazotumiwa na China katika kuharakisha mchakato wa kuleta maendeleo na mambo ya kisasa (modernization drive).

  Kuna idara maalum ya serikali (State Administration of Foreign Experts Affairs) inayoshughulikia mambo yanayohusu wataalamu kutoka nje, ikiwa ni pamoja na kuainisha maeneo yenye mahitaji ya wataalamu kutokana nje na hata wafanyakazi wasio wataalamu kutoka nje.

  Idara hiyo licha ya kushughulikia vibali vya ukazi, makazi na mambo mengine yanayohusu kuwaleta wageni hao kufanya kazi China, pia ina utaratibu wa kukusanya maoni na mapendekezo kutoka kwa wataalamu na wafanyakazi wageni kimaandishi na kuyafikisha kwa watunga sera na wahusika katika idara mbalimbali.

  Zaidi ya hayo, China ina mkakati kabambe ulioanza mwaka 2008 unaoitwa "vipaji 1000", wenye lengo la kuwavutia wachina hodari elfu moja hasa wale waliokwenda kusoma nje warudi nyumbani.

  Mpango huu unawalenga zaidi wachina na watu wenye asili ya China, ambao ni watafiti na waliopata shahada ya uzamivu hasa kwenye nchi za magharibi.

  Serikali imeweka mazingira mazuri ya kazi, malazi, vitendea kazi na malipo mazuri kwa wataalamu wenye asili ya China wanaorudi China na wale wasio na uraia wa China wanapewa hadhi ya ukazi ya wachina wanaorudi nyumbani, ili kuwaondolea vikwazo vyote vinavyoweza kuleta ugumu kwa wao kufanya kazi.

  Ujenzi wa pampu za kuhifadhia maji ukiendelea nchini

  Nilibahatika kuongea na raia wa Marekani mwenye asili ya China, Mdenmark mwenye asili ya China na Mchina kutoka Hong Kong, ambao walinieleza jinsi serikali ilivyowawekea utaratibu mzuri na rahisi unaohusiana na maswala ya ukazi kwao kutokana na wao kutokuwa na pasipoti za China.

  Kuvutia wataalam si jambo jipya China

  FikraPevu ilimkariri Waziri Mkuu wa hapa China, Li, akieleza jinsi wataalamu wageni wanavyosaidia kuleta mambo ya kisasa hapa China, nilikumbuka na kuanza kujiuliza kuhusu mpango tuliowahi kuwa nao Tanzania wakati wa enzi za awamu ya kwanza na ya pili.

  Tuliwahi kuwa na wataalamu wageni inawezekana baadhi bado wapo, ulikuwa na mabwana shamba na hata wataalamu wa afya, lakini leo wataalamu hao hawaonekani, hata wale tuliowaita ma-TX kama wale kutoka mashirika ya misaada ya nchi za Ulaya Kaskazini NORAD na DANIDA hawapo. Ninachokiona kwa sasa ni kitu kama ni udhaifu katika kuweka mazingira mazuri ya kuwafanya wataalamu wageni waendelee kubaki Tanzania.

  Kuyeyuka kwa wataalamu Tanzania

  Kibaya zaidi ni kuwa hata wataalamu wetu wachache waliopewa mafunzo Tanzania au waliogharamiwa na serikali ya Tanzania, wanakimbilia nje ya nchi.

  Kuna wakati aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya Dr Aisha Kigoda, alisema kati ya wataalamu wa afya 342 wa Tanzania, zaidi ya 110 walihamia nchi za Kusini mwa Afrika zenye mazingira mazuri zaidi ya kazi kuliko Tanzania. Hali sio tu ipo kwenye sekta ya afya, kuna wahandisi watanzania waliokimbia nchi yetu, kuna watafiti na hata wahadhiri waandamizi waliochagua kubaki katika nchi za magharibi, kwa kuwa nchi hizo zimewapa mazingira mazuri kuliko nchi yetu.

  Pamoja na kuwa wachina wanasifika kwa kuchapa kazi, wanatambua kuwa mchango wa wataalamu kwenye maendeleo ni muhimu. Tunatakiwa tukumbuke kuwa katika zama hii ya sayansi na teknolojia bila kuwa na mpango maalumu wa kuvutia wataalamu wageni na kuwafanya wabaki Tanzania, kuweka mazingira mazuri kwa watanzania wanaosoma nje kurudi nyumbani, na hata kuhakikisha wachache waliosoma na kubaki Tanzania hawaendi kwenye nchi nyingine, maendeleo ya Tanzania katika sekta nyingi yataendelea kuwa nyuma.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako