• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • CPC-China kuimarisha mahusiano na Vyama vya siasa Afrika kwa kujikita kwenye maendeleo ya wananchi

    (GMT+08:00) 2017-05-05 14:23:58
    Na Theopista Nsanzugwanko, Beijing

    USHIRIKIANO wa China na nchi za Afrika umekuwa ukiimarika kila kukicha katika masuala mbalimbali ya kiuchumi,kiteknolojia, kiusalama na mengineyo katika kuhakikisha uhusiano unaimarika katika Nyanja tofauti.

    Hivi karibuni katika kuhakikisha uhusiano unazidi kuwa imara Africa na China walisaini makubaliano ya ushirikiano (FOCAC), katika mkutano uliofanyika mwaka 2015 nchini Afrika Kusini na tayari nchi 46 kati ya 54 za Bara la Afrika zimeridhia mkataba huo.

    Mkataba huo wa ushirikiano uliendana na makubaliano ya kupokelewa kwa dola bilioni 60 kama kwa nchi za Bara la Afrika na mikopo mingine tofauti kutoka benki za kibiashara nchini China, pia uanataka kuimarisha mahusiano katika Nyanja tofauti.

    Hivyo kumekuwa na mahusiano yaliyo bora ya kisiasa ambapo Chama tawala cha Kikomunisti cha China (CPC), kimeeleza kuzidi kuimarisha ushirikiano na vyama vya siasa Afrika kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na kuleta maendeleo.

    Chama hicho cha CPC, kilichofanikiwa kufikisha nchi ya China katika maendeleo ya kiuchumi kwa muda mchache kimedhamilia kusaidia nchi za Afrika katika kuweka mifumo imara ya kisiasa kwa ajili ya kupatia maendeleo ya nchi hizo.

    Katika ushirikiano na vyama vya siasa na nchi za Afrika, CPC bila kujali tofauti za mifumo kimedhamilia kuendeleza na kupanua ushirikiano na vyama vya siasa Afrika.

    Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Afrika katika kamati kuu CPC , Xiangyang Gao anasema uhusiano baina ya chama hicho na vyama vya siasa ulianza tangu miaka ya 50s wakati nchi za Africa zinapambana kupata uhuru na kila siku umekuwa ukiimarika .

    Anasema CPC ina ushirikiano na vyama vya siasa zaidi ya 60 katika nchi hizo na kati ya hivyo 30 vikiwa vyama tawala na mpaka sasa wamekuwa wakiweka mikakati mbalimbali yakuimarisha mahusiano.

    "Katika mahusiano haya yako katika nyanja tofauti, lakini kwa lengo la kuhakikisha vyama husika vinapata fursa ya kujifunza baina ya pande zote mbili na kubadilisha uzoefu kwa lengo la kuletea wananchi maendeleo,na mahusiano haya yamekuwa imara na kuongezeka kila wakati"anasema

    Anaweka bayana kuwa bila kujali mfumo unaotumika katika nchi za kiafrika ikiwa ni kikomunisti au kibepali wamekuwa na mahusiano na vyama vya siasa vikiwemo vyama vikongwe na vingine vipya katika medali ya siasa Afrika.

    "CPC inaheshimu uhuru wa kila chama cha siasa katika kujenga na kuimarisha mahusiano yao iwe kipo katika utawala au la huku chama kikiwa huru kuchagua mfumo wanaotaka, jambo ambalo haliathiri mahusiano yetu"anasema.

    Suala muhimu siyo aina ya mfumo wa siasa haijalishi ni mfumo gani bali ni kuhusu maendeleo ya nchi husika kwani agenda kuu kwa sasa katika nchi za Afrika ni maendeleo ya nchi husika katika masuala ya kisiasa, kiuchumi, viwanda na kilimo.

    "CPC tunachofanya ni kusaidia nchi za afrika katika masuala ya maendeleo,katika kushirikiana katika masuala mbalimbali kwa kutumia vyama hivyo vya siasa vyenye uhusiano mzuri nasi ikiwa ni pamoja na kuwaeleza kile tunachofanya na kusaidia kuleta maendeleo ,kama itawapendeza nao kutumia'anasema

    Anaeleza kuwa jambo muhimu na malengo ya mahusiano baina ya CPC na vyama vya siasa Afrika ni kuangalia namna ya kutumia vyama hivyo kuleta maendeleo ya nchi.

    Anaweka wazi kuwa CPC inavichukulia vyama vyote vyenye mahusiano nao kuwa ni sawa bila kujali ukubwa au udogo na kuheshimiana kwa kukubaliana na tofauti zitakazokuwepo.

    Katika mahusiano na vyama vya siasa, CPC hawaingilii masuala ya ndani ya chama au nchi na kamwe hawatumii mahusiano baina yake na chama cha siasa kuingilia masuala ya kiserikali.

    "Katika mahusiano yetu na vyama vya siasa katika nchi mbalimbali Afrika,kamwe hatutumii kuingilia masuala ya ndani ya chama ,nchi na hata serikali"anasisitiza

    Anasema katika masuala ya fedha, bunge la nchi imekuwa ikipitisha bajeti katika kusaidia vyama vya siasa katika nchi za afrika ikiwemo kuwajengea uwezo wanachama wa vyama hivyo pamoja na kusaidia masuala mbalimbali ya kiofisi,ikiwemo kusaidia vifaa vya ofisi za vyama na mengineyo.

    Anasema katika kukuza ushirikiano, baadhi ya wajumbe wa chama cha CPC wamekuwa wakialikwa katika mikutano mikubwa ya vyama hivyo vya siasa kama vile ANC nchini Africa Kusini na Chama cha Mapinduzi (CCM ) nchini Tanzania.

    Lakini pia wajumbe kutoka CPC, wamekuwa wakitembelea nchi za Afrika kwa nyakati tofauti na kukutana na viongozi na wanachama ambapo wanapata fursa ya kubadilishana mawazo hususan kuhusu CPC na mafanikio yake ya kisiasa katika kuleta maendeleo ya nchi.

    "Pia, tumekuwa tukifanya mikutano kwa ajili ya kuwaandaa viongozi wa kisiasa wa China na Afrika wenye umri mdogo na kwa mara ya kwanza ulifanyika nchini Namibia mwaka 2012 na mkutano wa Pili ulifanyika mwaka 2015 Arusha, Tanzania" anasisitiza.

    Katika kuimarisha ushirikiano baina ya CPC na Chama tawala nchini Tanzania (CCM) mwezi Machi mwaka huu ujumbe wa watu 19 kutoka chama hicho ulifanya ziara ya siku tatu nchini Tanzania.

    Ujumbe huo ulioongozwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CPC, Guo Jin Long ulifanya mazungumzo na Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli, naMakamu Mwenyekiti wa CCM, Dk Ali Mohamed Shein.

    Gao anasema ziara kama hizo, zimekuwa zikifanyika katika nchi nyingine za afrika na kufanya mazungumzo au mkutano na viongozi na wanachama wa vyama hivyo kwa kuzingatia Agenda maalum watakayokuwa wamekubaliana.

    Mbali na ujumbe kutoka CPC kutembelea nchi za Afrika, lakini pia kuna wakati viongozi,wabunge au watendaji wa vyama rafiki utembelea China na kujifunza masuala mbalimbali.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako