• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Vijiji vya mlimani vyaondoa na umaskini kutokana na kilimo cha mitishamba

    (GMT+08:00) 2017-07-05 16:32:50

    Mji mdogo wa Yangba mjini Longnan mkoani Gansu China una mashamba ya kuvutia, milima na misitu ya kupendeza, na hali ya hewa ya kawaida. Mazingira ya kipekee na hali ya hewa nzuri si kama tu vimewapatia wakazi wa huko raslimali nyingi za asili, bali pia zinafaa kwa kilimo cha mitishamba aina ya Gastrodia Elata. Lakini milima mirefu pia imesababisha hali duni ya barabara. Ni vigumu kwa wanakijiji kupeleka na kuuza mazao yao sokoni, hivyo wamekuwa wanasumbuliwa na umaskini katika miaka mingi iliyopita, kama wimbo unavyoeleza,

    "Kijiji kiko mlimani, katika mamia ya miaka iliyopita, hakijawahi kuwasiliana na nje. Matofaa matamu, pilipili nyekundu, na uyoga mweusi haviwezi kuuzwa nje ya milima, kweli hatujui la kufanya…"

    Mjini Yangba kuna shirikisho dogo la kilimo cha mitishamba ya Gastrodia Elata. Shirikisho hilo lililoundwa mwaka 2004, linashughulikia uzalishaji na utengenezaji wa bidhaa za Gastrodia Elata, pia linatoa huduma za ufundi wa kilimo cha mitishamba hiyo kwa wakulima. Hivi sasa lina zaidi ya hekta 800 za mitishamba na wajumbe zaidi ya 800. Kila siku meneja mkuu wa shirikisho hilo Bw. Li Manfu anakwenda kwenye ofisi yake mapema, kuwapatia wakulima ujuzi wa kilimo cha mitishamba, na kujadiliana nao kuhusu namna ya kuongeza uzalishaji.

    "Unatakiwa kutia kuvu inayosaidia ukuaji wa mitishamba kuanzia pande mbili hadi katikati, hatua hii inasaidia Gastrodia Elata ziwe kubwa zaidi. Kwa kawaida zile kubwa zinakuwepo pande mbili na zile dogo zinakuwepo katikati, sivyo?"

    "Nafanya majaribio ya ujuzi mpya, nitautumia pamoja na ujuzi wa zamani, ili kuona ni njia ipi ina uzalishaji mkubwa."

    Mwanakijiji Liu Yucheng mwenye umri wa miaka 53 ni mjumbe aliyeshiriki mapema zaidi kwenye shirikisho la kilimo cha Gastrodia Elata. Kabla ya hapo alikuwa mfanyakazi wa mgodi wa shaba wa Yangba. Mwaka 2004 alipoteza kazi yake. Familia yake ilikuwa inashughulikia kilimo cha mitishamba hiyo, lakini haikuweza kupata mavuno makubwa, tena alitakiwa kulea watoto wawili, hivyo alikabiliwa na shinikizo kubwa la kiuchumi. Kuundwa na shirikisho hilo kulimpatia matumaini ya kuondokana na umaskini.

    "Zamani tulipolima Gastrodia Elata, hatukuwa na ujuzi. Baada ya shirikisho letu kuundwa, meneja Li alitupatia Gastrodia Elata ya aina nzuri, na kutuma wataalamu kutupatia ujuzi husika, mavuno ya mitishamba hiyo yanaongezeka hatua kwa hatua. Aidha, shirikisho hilo linaagiza mitishamba tunayozalisha kwa bei ya juu na kuuza kwa pamoja. Zamani tuliweza kupata yuan elfu kadhaa tu, lakini sasa tunaweza kupata mapato zaidi ya yuan elfu 17. Kimsingi tumeondokana na umaskini."

    Mwanakijiji Gu Huailiang mwenye umri wa miaka 47 pia ni mjumbe aliyeshiriki mapema zaidi kwenye shirikisho hilo. Kabla ya hapo aliishi katika nyumba ya udongo, wazazi wake wenye umri wa miaka zaidi ya 80 hawana afya nzuri, na watoto wake wawili wenye umri wa miaka zaidi ya 10 bado wanasoma. Shinikizo kubwa la maisha lilimfanya awe na wasiwasi kubwa. Siku hizi si kama tu amekuwa mkulima hodari, bali pia amekuwa msaidizi wa meneja Li kuhusu mauzo ya mitishamba wa.

    "Zamani tulipanda aina mbaya ya mitishamba kwa njia ya jadi, hivyo uzalishaji ulikuwa mdogo. Shirikisho letu limetusaidia kupanda Gastrodia Elata chotara na kutumia kuvu inayosaidia ukuaji wa mitishamba hiyo, sasa uzalishaji na mapato yetu yote umeongezeka. Zamani tuliweza kupata yuan elfu tano hivi, sasa licha ya kilimo cha mitishamba, pia naweza kupata yuan elfu 10 kwa kufanya biashara na meneja Li, kwa ujumla naweza kupata yuan elfu 40 hadi elfu 50."

    Meneja Li Manfu wa shirikisho hilo pia naye aliwahi kupoteza ajira. Alianzisha shirikisho lake kwa kushirikisha wafanyakazi wengine waliopoteza ajira. Baada ya kupata maendeleo kwa zaidi ya miaka 10, siku hizi shirikisho hilo limekuwa kampuni muhimu ya mauzo ya mazao ya kienyeji ya mji mdogo wa Yangba. Kuwajibika na jamii na kunufaisha wakazi wote wa huko ni wazo la shirikisho hilo. Bw. Li Manfu anasema,

    "Shirikisho letu likiwa ni kampuni inayonufaika na sera husika za serikali, linatakiwa kuwajibika kwa jamii na kutoa fedha kuwasaidia watu maskini. Kila mwaka tunazisaidia familia 50 zenye matatizo ya kiuchumi kutoka vijiji vitatu vilivyoko mlimani."

    Ili kuwasaidia wakulima maskini kuinua uwezo wa uzalishaji, shirikisho hilo linawapatia mbegu za aina nzuri na mbolea bila malipo, kuwapatia huduma za mafunzo, na kuagiza mazao kwa bei ya juu. Kiongozi anayeshughulikia ununuzi wa Gastrodia Elata Bw. Xiao Yuguo alipotaja hatua mbalimbali za kuwasaidia wakulima, alisema,

    "Mwaka jana meneja Li aliagiza tani 90 za mbegu za Gastrodia Elata chotara, tuliwapa wakulima mbegu hizi bila malipo. Pia tunawapa kuvu inayosaidia ukuaji wa mitishamba hiyo. Tunapoagiza mitishamba kutoka kwa wakulima, tunalipa yuan 16 kwa kilo, wakati wafanyabiashara wengine wanalipa yuan 14 tu kwa kilo."

    Shirikisho la kilimo cha Gastrodia Elata la Yangba si kama tu limewapatia wakulima mbegu za aina nzuri na utaalamu wa kilimo, bali pia limewasaidia kuuza mazao yao kwenye soko lenye ushindani mkubwa. Shirikisho hilo limetatua matatizo ya mauzo ya wakulima hao kupitia biashara inayofanyika kwenye mtandao wa Internet. Na maendeleo ya biashara kwenye mtandao wa Internet pia yamewahimiza wanakijiji wengi zaidi kushiriki kwenye shughuli husika, ikiwemo kuanzisha maduka ya mitishamba kwenye mtandao wa Internet.

    Bibi Wang Xiaoqin ni msichana mchangamfu, aliwahi kufanya kazi ya kibarua katika kiwanda cha elektroniki mjini Shenzhen mkoani Guangdong, lakini mshahara wa kiwandani ulikuwa mdogo, na mji wa Shenzhen uko mbali sana na maskani yake, hivyo alirudi nyumbani na kuanza kuuza bidhaa za shirikisho la kilimo cha Gastrodia Elata kupitia mtandao wa Internet. Sasa amekuwa mmiliki hodari wa duka kwenye mtandao. Anasema,

    "Zamani nilifanya kazi ya kibarua nje ya kijiji, sasa nimerudi nyumbani kuendesha duka kwenye mtandao. Hapa ni kivutio cha utalii, nilitaka kuwafahamisha watalii mazao ya kienyeji ya hapa, hivyo nilianzisha duka kwenye mtandao, sikujua kama mauzo kupitia mtandao wa internet ni makubwa zaidi kuliko duka halisi. Sasa mauzo kupitia mtandao kwa mwezi ni yuan elfu 10 hadi elfu 20. Kufanya kazi nyumbani ni kuzuri, tena naweza kuwasaidia wakazi wa hapa kuuza mazao ya kienyeji na kuongeza mapato yao."

    Bibi Wang Xiaoqin alipotaja msaada wa shirikisho la kilimo cha Gastrodia Elata kwa duka lake, alifurahi sana.

    "Zamani nilitakiwa kuagiza mazao kutoka kwa mkulima mmoja mmoja, na uzalishaji wa mazao haukuweza kuhakikishwa. Sasa sina haja kwenda mbali, naweza kuagiza bidhaa mbalimbali kwa urahisi kutoka kwa shirikisho hili. Shirika hili lilitengeneza bidhaa za Gastrodia Elata kwa mujibu wa vigezo vya taifa. Baadhi ya wafanyabiashara wanatia Sulfur wanapotengeneza mitishamba, lakini shirikisho hilo halitumii kemikali yoyote, hivyo viwanda vingi vya dawa vinaagiza bidhaa hapa. Nilisikia mfanyakazi wa kiwanda cha dawa cha mkoa wa Zhejiang akisema upimaji unaonesha Gastrodia Elata zetu zina sifa nzuri zaidi."

    Katika mji mdogo wa Yangba, mitishamba ya Gastrodia Elata imeunganisha wakulima maskini, wafanyakazi waliopoteza ajira na watu waliowahi kufanya kazi za vibarua nje. Gastrodia Elata si kama tu ni mitishamba mizuri inayotibu ugonjwa wa kizunguzungu, bali pia ni dawa ya kuondoa umaskini. Na kama wimbo unavyosema, hii ni zama ya biashara kupitia mtandao wa Internet, maendeleo ya biashara kupitia mtandao wa Internet yamewafanya watu wengi zaidi kujua mitishamba hiyo, hata imeuzwa nchini Japan, Korea Kusini na Russia, na kuwafanya wanakijiji wa huko kutajirika siku hadi siku.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako