Mtoto Ashtakiwa Baada Ya Kumsaidia Mzee
2020-08-21 16:49:26| CRI

Mtoto Ashtakiwa Baada Ya Kumsaidia Mzee

Mzee Tang Qiu mwenye umri wa miaka 89 alivunjika mfupa baada ya kuanguka, lakini akamfungulia mashtaka mtoto mwenye umri wa miaka 11 anayejulikana kwa jina la Xiao Hao, na kumdai fidia ya Yuan laki 1.7.

Bibi Tang Qiu alisema, tarehe 12 mwezi Machi mwaka 2019 alipojaribu kuvuka barabara mwenyewe akitumia kiti cha magurudumu, mtoto Xiao Hao alimwona na ghafla akakimbia akikisukuma kiti chake kwa kasi, hali ambayo ilimshutua Bibi Tang Qiu. Baada ya kumwambia mara kadhaa mtoto huyo kusimama na kuacha kusukuma kiti, hatimaye Xiao Hao akasimama. Wakati Bibi Tang alipokuwa akijaribu kusimama kutoka kwenye kiti chake, kijana huyo alianza tena kusukuma kiti ili kujiburudisha, na kumgonga Bibi Tang ambaye alianguka chini.

Lakini kwa upande wa mshtakiwa, mtoto Xiao Hao alitoa maelezo tofauti ya tukio lilivyotokea siku hiyo. Alisema kuwa alikuwa anamsaidia bibi huyo kuvuka barabara, na wala sio kusukuma kiti chake cha magurudumu kwa kujiburudisha. Xiao Hao alieleza kuwa siku hiyo alipokuwa njiani kwenda shuleni, alimsikia Bibi Tang Qiu akimwambia "Nisukume nivuke barabara", kisha akaenda kumsaidia kusukuma kiti chake hadi afike upande mwingine wa barabara. Alisema, ni Bibi Tang alimwomba msaada, na mfanyakazi mmoja wa Supamaketi pia alitoa msaada, na kwamba yeye mwenyewe hana nguvu ya kutosha kumsukuma. Xiao Hao amesema baada ya kuvuka barabara, Bibi Tang alianguka mwenyewe baada ya kujaribu kusimama na kupanda ngazi, na yeye hakumgusa kabisa.

Mahakama iliyoshughulikia kesi hiyo ilitoa hukumu kuwa haikubali madai ya fidia aliyotoa Bibi Tang Qiu kwa mtoto Xiao Hao, ambaye hana hatia. Kitendo cha kijana huyo kujitolea kumsaidia mzee anayehitaji msaada kinastahili kusifiwa, na hakuna ushahidi wowote unaothibitisha kuwa Xiao Hao alifanya makosa katika kesi hiyo.