Mwanaume ataka mpenzi wake amrudishie fedha baada ya kuachana
2020-08-26 13:07:26| CRI

Mwanaume ataka mpenzi wake amrudishie fedha baada ya kuachana

Ni jambo la kawaida kwa watu kuanzisha uhusiano wa kimapenzi, na wakigundua kuwa uhusiano wao haufai kuendelea, basi wanaachana. Lakini inakuwaje kama upande mmoja ukitaka upande mwingine urudishe fedha zilizotumiwa wakati wa uhusiano wa kimapenzi?

Bw. Xiao Wei na Bi Xiao Li walianzisha uhusiano wa kimapenzi mwaka 2018. Mwaka mmoja baada ya hapo Bi. Xiao Li alitaka kuachana na Bw. Xiao Wei. Lakini Bw. Xiao Wei aliona kuwa amemgharamia sana Bi. Xiao Li na kumtaka amrudishie fedha hizo, na pia alimfungulia mashtaka kumtaka alipe fidia ya RMB yuan laki 1.3, sawa na dola za kimarekani elfu 18.

Kwenye orodha yake ya matumizi ya fedha aliyoitoa Xiao Wei mahakamani, manunuzi ya vyakula, matunda, vitafunwa, tiketi za filamu, gharama za kupanda gari na ndege zote zimehusishwa, na gharama ya chini zaidi ni yuan nane ya gharama ya mawasiliano, sawa na dola moja za kimarekani.

Fedha nyingine anazotaka Xiao Li kurudishiwa zinahusisha gharama za manunuzi ya bidhaa za kidijitali, mapambo ya nyumba, na fedha alizompa kupitia kadi za mikopo, na gharama ya chini zaidi ni yuan 18.9, sawa na dola 2 za kimarekani, za kununua kitamaa cha jikoni.

Baada ya uratibu wa mahakama, Xiao Wei na Xiao Li walifikia makubaliano kwa hiari, na Xiao Li atalipa yuan elfu 40, sawa na dola za kimarekani elfu 6, kwa mikupuo miwili kabla ya muda uliopangwa, na pande hizo mbili hazitakuwa na mikwaruzano ya kifedha katika siku za baadaye.