Kijana mwenye umri wa miaka 18 apatwa ugonjwa wa jongo (gout) kutokana na kupenda kunywa vinywaji vyenye sukari
2020-09-08 11:47:31| CRI

Kijana mwenye umri wa miaka 18 apatwa ugonjwa wa jongo (gout) kutokana na kupenda kunywa vinywaji vyenye sukari

Hivi karibuni kijana mwenye umri wa miaka 18 kutoka mji wa Foshan, mkoani Guangdong, alipelekwa hospitali kutokana na kupendelea vinywaji vyenye sukari. Aligunduliwa kupatwa ugonjwa wa jongo la dharura baada ya kufanyiwa upimaji.

Lakini ni kwa nini kijana mwenye umri mdogo anapatwa ugonjwa huo? Daktari wa Hospitali ya Foshan alimwuliza kuhusu mwenendo wa maisha yake ya kawaida akagundua kuwa, kuna uwezekano kuwa kijana alipatwa ugonjwa huo kutokana na tabia yake ya kupendelea vinywaji venye sukari, na anakunywa vinywaji kama hivyo mara kadhaa kila wiki.

Ingawa Xiao Wang bado ni kijana, lakini ugonjwa wa jongo umemdhuru, anashindwa kutembea vizuri. Linalowatisha watu zaidi ni kuwa, viungo vyake vya mikono na miguu vimejaa dalili za jongo ambazo zinaonekana kama mawe.

Daktari Zheng ameeleza kuwa kiwango cha Asidi ya uric Xiao Wang alipopelekwa hospitali kilikuwa mara mbili kuliko kile cha kawaida kwa watu wazima wanaume. Na baada ya kufanyiwa matibabu, sasa Xiao Wang amepona na kuondoka hospitali.

Katika miaka ya hivi karibuni watu wengi wenye umri mdogo wanapatwa ugonjwa wa jongo. Madaktari wanapendekeza kuwa ili kujikinga dhidi ya kiwango cha juu cha Asidi ya uric, na kupatwa ugonjwa wa jongo, jambo muhimu kwa vijana ni kupunguza matumizi ya vinywaji vyenye sukari, kufanya mazoezi ya mwili, na kula vyakula vya aina nyingi, ili kuwa na afya njema.