Baba Amtupa Mtoto Wake Mchanga Karibu na Pipa la Taka
2020-09-10 12:32:49| CRI

Baba Amtupa Mtoto Wake Mchanga Karibu na Pipa la Taka

Mwanamume mmoja wa China mwenye umri wa miaka 24 amemtupa mtoto wake wa kike karibu na pipa la taka.

Picha ya video iliyorekodiwa na kamera za usalama za polisi inaonesha kuwa baba wa mtoto huyo Bw. Zhang, akitembea kuelekea kwenye kituo cha kukusanya takataka, akiwa na mtoto huyo mikononi siku hiyo alfajiri.

Bw. Zhang na mkewe, Bibi Li mwenye umri wa miaka 21, wanashikiliwa na polisi baada ya kukiri kumtupa binti yao.

Mtoto huyo aligunduliwa karibu na kituo kimoja cha kukusanya takataka kwenye eneo le makazi mjini Dongguan mkoani Guangdong, asubuhi ya Julai 29. Mtoto huyo alipelekwa hospitali na upimaji unaonesha kuwa yuko katika hali nzuri ya kiafya. Baadaye alipelekwa kwenye Kituo cha Huduma za Kijamii cha Mji wa Dongguan ili atunzwe kwa siku iliyofuata.

Baada ya kuhojiwa na polisi, wanandoa hao walikiri kumtupa mtoto wao muda mfupi baada ya kuzaliwa. Bw. Zhang na Bi. Li walisema mtoto huyo alizaliwa nyumbani saa saba usiku wa Jumatano, na waliamua kutomtaka huyo mtoto baada ya majadiliano mafupi, lakini hawakutaja sababu ya kufanya hivyo.

Baadaye Bw. Zhang alikwenda na binti yake mchanga karibu na pipa moja la taka na kisha kumwaacha pale.

Polisi wamemtia mbaroni Bw. Zhang kwa tuhuma za kutupa mtoto, na mke wake ameachiwa kwa dhamana akisubiri kesi yake ya mashtaka hayohayo kusikilizwa.