Yaya Apigwa Picha Akimpiga Mtoto Mchanga
2020-09-11 11:46:15| CRI

Yaya Apigwa Picha Akimpiga Mtoto Mchanga

Yaya mmoja nchini China amerekodiwa kwa picha ya video na kamera ya usalama nyumbani akimpiga mtoto mchanga mwenye umri wa siku sita. Baba wa mtoto huyo Bw. Tian amewaambia polisi kuwa alishtuka sana baada ya kutazama video hiyo kupitia simu yake ya mkononi wiki iliyopita.

Yaya huyo mwenye umri wa miaka 50 Bibi Wang, ameshtakiwa kwa tuhuma za kumpiga makofi na kumrusha mtoto huyo mchanga kama "toy".

Tukio hilo limezusha hasira kubwa kwenye jamii baada ya mama wa mtoto huyo kuweka video ya yaya huyu kwenye mitandao ya kijamii.

Mama huyo amedai kuwa yaya huyo alimtendea mtoto wake kwa mabavu wakati akimwangalia katika nyumba yao mjini Shahe mkoani Hebei, kaskazini mwa China. Polisi mjini Shahe wameanzisha uchunguzi kuhusu kesi hiyo baada ya video kutangazwa mitandaoni Jumatatu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na polisi, Bw. Tian amedai kuwa amewahi kumuona Bibi Wang akimpiga mtoto wake mikononi, miguuni na matakoni kupitia kamera ya usalama aliyoiweka nyumbani kwake.

Bw. Tian alisema aligombana na yaya huyo baada ya kugundua alichofanya dhidi ya mtoto wake siku hiyo. Halafu alienda kwa wakala wake wa huduma za nyumbani kulalamika kuhusu vitendo vyake siku iliyofuata.

Polisi wamesema kuwa yaya huyo alipojaribu kuondoka kwa gari lake, Bw. Tian aliyekasirika sana alitumia nyenzo kuharibu gari la Bibi Wang, hali ambayo ilimshtua sana na akapelekwa hospitali. Maofisa wa Polisi wamesema uchunguzi unaendelea, na kesi hiyo inashughulikiwa kama kesi ya madai na sio ya jinai.