Rais wa China ahutubia mkutano wa viongozi wa viwanda na biashara wa APEC
2020-11-19 18:12:37| cri

Rais wa China ahutubia mkutano wa viongozi wa viwanda na biashara wa APEC

Rais Xi Jinping wa China leo amehudhuria na kuhutubia mkutano wa viongozi wa viwanda na biashara wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Asia na Pasifiki (APEC) uliofanyika kwa njia ya video. Rais Xi amesisitiza kuwa dunia ni jumuiya isiyotengeka yenye hatma ya pamoja, na nchi mbalimbali zinapaswa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kwenye mapambano dhidi ya janga la virusi vya Corona na kuhimiza ufufukaji wa uchumi wa dunia. 

Kwenye hotuba yake inayoitwa “kujenga muundo mpya wa maendeleo na kutimiza ushirikiano wa kunufaishana”, Rais Xi Jinping amebainisha kuwa janga la virusi vya Corona limethibitisha mara nyingine tena kuwa  maslahi ya nchi mbalimbali yanategemeana kwa karibu, na dunia ni jumuiya isiyotengeka yenye hatma ya pamoja.

“Nchi zote zinapaswa kujaliana na kusaidiana, kushirikiana na kushikamana, kuongeza mawasiliano na uratibu wa kisera, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kwenye mapambano dhidi ya virusi vya Corona, ili tuweze kulishinda mapema janga hilo, na kutimiza ukuaji endelevu na shirikishi na wenye uwiano wa uchumi wa dunia.”

Rais Xi amesisitiza kuwa mwelekeo mzuri wa maendeleo endelevu ya uchumi wa China haujabadilika. China itatekeleza kithabiti wazo jipya la maendeleo na kujenga muundo mpya wa maendeleo. Anasema,

“Kamwe hatutarudi nyuma kwenye historia, hatutafuti ‘kutengana’ na nchi yoyote au kujenga ‘mzunguko mdogo’ wa marafiki mahususi. Muundo wetu mpya wa maendeleo kamwe hautakuwa mzunguko wa ndani unaofunga mlango kwa nje, bali ni mizunguko miwili ya ndani na kimataifa iliyo wazi na yenye kuhimizana.”

Rais Xi ameainisha kuwa chini ya muundo mpya wa maendeleo, soko la China litaweza kuonesha uwezo wake kamili na kutimiza mahitaji mengi zaidi kwa nchi mbalimbali duniani.

“Tutapunguza zaidi viwango vya ushuru na gharama za kimfumo, kuanzisha maeneo maalumu kwa ajili ya kuhimiza biashara ya nje, na kuongeza uagizaji wa bidhaa na huduma zenye ubora wa hali ya juu kutoka nchi mbalimbali. Naamini kuwa kutokana na soko la China kuendelea kupanua uwezo wake, litatoa fursa nyingi zaidi kwa nchi mbalimbali, na kutia msukumo mkubwa zaidi kwa maendeleo ya uchumi wa dunia.”

Rais Xi amesema chini ya muundo mpya wa maendeleo, China itaendelea kufungua mlango zaidi na kupanua ushirikiano na nje, na kutimiza lengo la kunufaishana na nchi mbalimbali duniani.

“Tutajituma zaidi kushiriki kwenye mgawanyo wa kazi wa kimataifa, kuingia kwa ufanisi zaidi kwenye minyororo ya viwanda, ugavi na thamani duniani, na kupanua zaidi mawasiliano na ushirikiano na nje. Nchi, sehemu na kampuni yoyote inayotaka kushirikiana na China, tutapenda kufanya ushirikiano nayo.”Rais Xi amesema, China itaendelea kushikilia mfumo wa pande nyingi na kanuni ya kujenga kwa pamoja, kujadili kwa pamoja na kunufaika kwa pamoja, kusukuma mbele ujenzi wenye ubora wa juu wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, na kuimarisha ushirikiano wa maendeleo yasiyoleta uchafuzi kwa mazingira.