SOKA: Gerard Pique kukaa nje ya uwanja kwa miezi sita
2020-11-23 16:48:42| cri

Gerard Pique anatarajia kukaa nje ya uwanja kwa miezi sita baada ya kuumia kwenye mchezo wa juzi. Mkongwe huyo wa Barcelona alitoka nje ya uwanja akiwa mwenye majonzi baada ya kuumia goti la mguu wa kulia wakati Barca ikilala kwa bao 1-0 dhidi ya Atletico Madrid kwenye mchezo wa La Liga. Aliumia alipogongana na nyota wa Atetico, Angel Correa na mguu kugeuka vibaya, licha ya kusaidiwa kwa matibabu ya uwanjani lakini alitolewa uwanjani. Kipigo hicho ni cha tatu kwa Barca msimu huu na kuiacha miamba hiyo na pointi tisa nyuma ya vinara wa LaLiga, ikiwa nafasi ya 10 kwenye msimamo wa La Liga unaoongozwa na Real Sociedad. Hilo ni pigo kwa kocha Ronald Koeman, ambaye atakuwa na kikosi bila ya kuwa na kiongozi wa safu ya ulinzi kwa miezi sita sasa, kwa mujibu wa gazeti la Hispania la Sport. Yannick Carrasco alifunga bao pekee la mchezo huo, akitumia makosa ya kipa Marc Andre ter Stegen. Mambo yakawa mabaya zaidi kwa Barca wakati Pique akiumia kipindi cha pili akiangukiwa na Correa, tatizo ambalo linamfanya nyota huyo wa zamani wa Man United mwenye miaka 33 kukaa nje. Taarifa zinadai kuwa goti lake liliumia vibaya, wakati Barca akidai kuwa maumivu ya nyota huyo si makubwa na atatakiwa kufanyiwa uchunguzi wa mara nyingine kuangalia tatizo lake