WAKAZI WA KWALE WASHAURIWA KUTUMIA MBINU ZA SASA ZA KILIMO
2020-11-23 18:09:39| cri

 

Serikali ya Kaunti ya Kwale imewashauri wakazi kujihusisha na shughuli za kilimo ili kuepuka kutegemea vyakula vya misaada nyakati za kiangazi.

Kaunti hiyo iliwataka wakazi wake kutumia mbegu bora na usaidizi unaotolewa na serikali kwa wakulima kuboresha mazao yao.

Naibu wa gavana katika kaunti hiyo Bi Fatuma Achani alisema kaunti imeweka mikakati kabambe kuhakikisha kuwa wakulima wanahamasishwa kuingilia kilimo cha kisasa kitakachosaidia kuongeza mazao. Alisema tangu kuingia kwa janga la corona nchini watu wengi ambao walikuwa wameajiriwa katika sekta ya utalii walipoteza ajira kufuatia kufungiwa kwa ndege kutoka mataifa ya kigeni hivyo kilimo biashara kitawasaidia kujikimu kimaisha.

Aliongezea kuwa baada ya kukamilika kwa soko la Kombani wakazi wataweza kupata soko la kuuzia mazao yao ambapo wafanyibiashara na wanunuzi kutoka kaunti zingine watafika hapo kununua.

Alisema kaunti hiyo imekuwa ikiwasaidia wakulima mashinani kwa kuwapa mbegu zilizo boreshwa, kuwapa usaidizi wa kifedha na kuwahamasisha kuhusiana na kilimo cha kisasa.

Alisema mwanzo wa Septemba serikali ya kaunti hiyo ilipeana mashine ya kupukuchua mahindi na mbegu za kisasa ambazo zilipangiwa kuwafaidi wakulima zaidi 12,000.