China yaondoa kaunti zote zilizobaki kwenye orodha ya umasikini
2020-11-23 18:32:51| cri

Serikali ya mkoa wa Guizhou leo Jumatatu imetangaza kuwa China imefanikiwa kuondoa kaunti zote zilizobaki kwenye orodha ya umasikini. Kaunti tisa za mwisho, ambazo zote zipo kwenye mkoa huo uliopo kusini magharibi mwa China, zimeondolewa kabisa kwenye umasikini. Mkurugenzi wa ofisi ya maendeleo na upunguzaji wa umasikini ya mkoa wa Guizhou, Li Jian amesema tathmini iliyofanywa na mashirika ya upande wa tatu mapema mwezi huu, inaonesha kwamba matukio ya jumla ya umasikini kwenye kaunti tisa za mkoa huo yamepungua hadi asilimia sifuri, na kiwango cha kuridhika cha wenyeji kilikuwa zaidi ya asilimia 99.

Wastani wa mapato ya watu masikini kwa mwaka kwenye kaunti hizi tisa yameongezeka hadi yuan 11,487 sawa na dola za kimarekani 1,740, ambazo ziko juu ya mstari wa umasikini wa yuan 4,000 kwa mwaka huu. China iliapa kutokomeza umasikini nchini kote hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2020. Mwishoni mwa mwaka 2019, kaunti 52 za kaskazini magharibi, kusini magharibi na kusini mwa nchi zilibaki kwenye orodha ya umasikini.