NDONDI: Promota wa Twaha Kiduku anasakwa na polisi kwa kuwatapeli mabondia
2020-11-24 16:55:02| cri

Inaelezwa kuwa promota wa pambano la ngumi za kulipwa kati ya Mtanzania, Twaha Kiduku na Sirimongkhon Lamthuam raia wa Thailand anatafutwa na polisi wa kituo cha Kilwa Road kufuatia madai ya kutowalipa mabondia fedha zao akiwemo Kiduku na watoa huduma wengine waliokuwepo katika pambano hilo lililochezwa mwezi uliopita.

Katika pambano hilo ambalo lilifanyika kwenye Ukumbi wa PTA jijini Dar, Kiduku alifanikiwa kuibuka na ushindi wa TKO ya raundi ya saba ambayo ilitokana na mpinzani wake kudai bega lake kushtuka kutokana na makonde makali ya Kiduku. Mabondia wote waliocheza kwenye pambano hilo, walikuwa wamelipwa malipo nusu na wengine hawakulipwa kabisa hali iliyosababisha promota huyo kuingia mitini na kila anapopigiwa simu hutoa sababu mpya. Baadhi ya mabondia waliokiri kumdai promota huyo anayetafutwa na polisi ni Juma Misumari na kocha wake kutoka Morogoro, Twaha Kiduku, Maono Ally na Jongojongo kutoka Bagamoyo na Alphonce Mchumia Tumbo.