Wanaouza saruji kwa bei ya ulanguzi Tanzania kufikishwa mahakamani,biashara zao kufungwa
2020-11-25 17:03:13| cri

Wafanyabiashara wanaouza saruji kwa bei ya ulanguzi nchini Tanzania watachukuliwa hatua za kisheria,ikiwamo kushtakiwa na kufungiwa biashara.

Onyo hilo limetolewa na serikali mkoani Morogoro,kutokana na bidhaa hiyo kuuzwa kwa bei ya juu.

Hayo yalibainishwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ,Loata Ole Sanare,wakati akizungumza na wafanyabiashara wa mkoa huo ,kuhusiana na kupanda kwa bei ya saruji bila sababu za msingi.

Sanare alisema serikali  itawafikisha mahakamani wafanyabiashara wote wanaouza bidhaa hiyo bei ya juu kwa kesi ya uhujumu uchumi.

Wafanyabiashara wamekuwa wakiuza bidhaa hiyo hadi shilingi 25,000 kwa mfuko mmoja wa kilo 50.

Sanare alisema serikali imefanya uchunguzi na kugundua kuwa manispaa ya Morogoro ndio inaongoza kwa kuuza saruji bei ya juu kulinganisha na maeneo mengine,jambo ambalo alisema haliwezi kukubalika.

Aidha alisema kuwa utaratibu wa kuwachukulia hatua wafanyabiashara utaanza baada ya uchunguzi kukamilika.

Aliongeza kuwa licha ya kufikishwa mahakamani,biashara zao pia zitafungwa.