NDONDI: Idd Pialali ‘Simba’ na Arnel Tinampay waanza kutambiana kufuatia pambano la Novemba 28
2020-11-25 16:12:23| cri

Kuelekea pambano kali la kimataifa la ngumi kati ya Bondia Mtanzania, Idd Pialali ‘Simba’ na Mfilipino Arnel Tinampay, mambo yamepamba moto, ambapo mabondia hao kila mmoja ametamba kuhakikisha anamkalisha mpinzani wake mapema tu kwenye pambano hilo litakalofanyika Novemba 28, mwaka huu kwenye ukumbi wa Next Door Arena jijini Dar es Salaam. Pialali amesema anataka kuwahakikishia kuwa hapa hakuna ushindi wa pointi ni lazima mtu akae kwa KO mapema tu ili wasije wakazoea, hivyo amejiandaa kumchakaza mapema huyo Mfilipino.

Naye Tinampay akijibu tambo hizo alisema anatamani mashabiki wake waanze kutangulia pale Next Door Arena leo hii kwa sababu kuna sapraizi ya burudani ya kutosha kwa ajili yao aliyoiandaa, Amesisitiza kuwa anajua Pialali ni bondia mzuri lakini tayari amemsoma na haitakuwa ngumu kumpiga. Pia siku hiyo litashuhudiwa pambano jingine la kimataifa kati ya bondia Mtanzania, Salim Mtango kutoka Tanga ambaye atapanda ulingoni kuzichapa na Eduardo Mancito wa Ufilipino.