Kenya-Kampuni ya LG yazindua barakoa mpya ya kisasa,yatoa barakoa 300 kwa wahudumu wa afya
2020-11-25 17:02:47| cri

Kampuni ya vifaa vya kielektroniki ya LG jana ilitangaza barakoa mpya jijini Nairobi,zilizotengenezwa kwa teknolojia ya kisasa.

Barakoa hizo zina uwezo wa kusafisha hewa wakati wa kupumua ili kumkinga mtumiaji dhidi ya kuvuta hewa chafu, ikiwemo hewa iliyo na viini vya virusi vya corona.

Barakoa hizo zina uwezo wa kusafisha hewa inayoingia kwenye pua ,na sehemu maalumu ya kuondoa hewa chafu mwilini mtu anapopumua.

Aidha barakoa hiyo ina betri ambayo hufanya kazi kwa muda wa saa nane kabla ya kuzima.

Wakati wa uzinduzi wa barakoa hizo,Kampuni ya LG ilitoa msaada wa barakoa 300 hizo mpya aina ya PuriCare zitakazosambazwa kwa madaktari nchini Kenya kupitia kwa Muungano wa wahudumu wa Kimatibabu (KMA).

Mkurugenzi Mkuu wa LG Afrika Mashariki, Bw Sa Nyoung Kim alisema barakoa za PuriCare zimetengenezwa ili kukidhi hitaji la vifaa ambavyo vinaweza kuwakinga watu dhidi ya virusi vya corona kote duniani.

Aliongeza kuwa barakoa hiyo inahakikisha kwamba anayeitumia anapumua vyema na kukingwa vizuri.

Kampuni hiyo ilitangaza kuwa barakoa zote 300 ilizotoa kwa wahudumu wa afya zina thamani ya Sh5 milioni , ikimaanisha kwamba kila barakoa inagharimu Sh17,000.

Kampuni hiyo ya LG inapanga kuanza kuuza barakoa hizo kote nchini mwaka 2021.