China yafanikiwa kutokomeza umaskini katika kaunti zote
2020-11-25 17:59:07| cri

Jumatatu wiki hii, serikali ya mkoa wa Guizhou ilitangaza kuziondoa kaunti tisa za mwisho kutoka kwenye orodha ya maeneo maskini ya mkoa huo, hatua ambayo inamaanisha kuwa kaunti zote maskini nchini China zimeondokana na tatizo hilo lililosumbua taifa la China kwa mamia ya miaka. 

Mwaka 2014, China ilitangaza orodha ya kaunti 832 zilizo nyuma kiuchumi, ambazo zinasambaa katika mikoa na miji 22. Wakati huo, kaunti maskini zilikuwa zinachukua nusu ya ardhi ya China, huku idadi yao ikichukua theluthi moja ya kaunti zote katika nchi nzima.

Tangu Mkutano mkuu wa 18 wa Chama cha Kikomunisti cha China ulipofanyika mwaka 2012, serikali ya China imeweka mkazo katika kazi ya kutokomeza umaskini, na kuichukulia kazi hiyo kama jukumu la msingi na kiashiria muhimu cha kukamilika kwa ujenzi wa jamii yenye maisha bora.

Kutokana na juhudi za pamoja na hatua madhubuti zilizochukuliwa na serikali kuu na serikali za mitaa, kuanzia mwaka 2016, kaunti maskini zimeanza kujikwamua kutoka kwenye tatizo hilo, na idadi ya kaunti zilizoondokana na umaskini kila mwaka ilifikia kilele mwaka 2019. Kwa miaka saba mfululizo, idadi ya watu waliotolewa kwenye umaskini kila mwaka nchini China imekuwa ikizidi milioni kumi, huku idadi ya jumla ya watu maskini kote nchini ikishuka kutoka milioni 98.99 ya mwaka 2012 hadi kufikia milioni 5.51 ya mwaka 2019.

Kutokomeza umaskini ni changamoto inayoikabili dunia nzima, na pia ni jukumu mhimu kwa nchi zinazoendelea. China ikiwa ni nchi inayoendelea yenye watu wengi zaidi duniani, mafanikio hayo iliyoyapata katika kupambana na umaskini yanatokana na mpango madhubuti uliowekwa na serikali kuu ya China na kujumuishwa kwenye Mkakati Mkuu wa Maendeleo ya Taifa. Muhimu zaidi ni kwamba China inayachukulia maendeleo kama mbinu ya msingi ya kumaliza umaskini, kutoa kipaumbele katika kuzijengea uwezo kaunti zilizo nyuma kiuchumi, na kutoa uungaji mkono wa kielimu na kifundi kwa kaunti hizo ili kuchochea msukumo wa ndani wa kutimiza maendeleo. Njia hiyo maalumu ya China ya kutokomeza umaskini imechangia busara ya China kwenye juhudi za kupunguza umaskini kote duniani, na kukubaliwa kwenye jamii ya kimataifa.

Naibu mkurugenzi wa Ofisi ya Kupunguza Umaskini ya Baraza la Serikali la China Bw. Xia Gengsheng amesema katika hatua ijayo, China itaendelea kuimarisha matokeo yaliyopatikana na kuweka mkazo katika kuendeleza na kustawisha maeneo ya vijijini kwenye kaunti zilizoondokana na umaskini, ili kusukuma mbele maendeleo ya jamii na kuboresha maisha ya watu kwenye maeneo hayo.