RAGA: Shujaa yapata mwaliko wa kucheza nchini Uhispania na Ufaransa
2020-11-26 18:33:11| cri

Timu ya taifa ya wanaraga saba kila upande almaarufu Shujaa, imepata mwaliko wa kucheza nchini Uhispania na Ufaransa mnamo Februari 2021, mwezi mmoja kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa kampeni za duru ya Raga ya Dunia. Mwenyekiti wa Shirikisho la Raga la Kenya (KRU), Oduor Gangla amethibitisha kwamba wamepata mialiko hiyo kutoka Uhispania na Ufaransa na ameeleza matumaini kwamba vipute hivyo vitakuwa sehemu muhimu ya maandalizi ya Shujaa kwa muhula mpya. Mbali na Kenya, vikosi vingine ambavyo vimealikwa kuchuana nchini Uhispania na Ufaransa ni New Zealand, Afrika Kusini, Australia, Fiji na Samoa. Kwa mujibu wa Gangla, washindani wa Shujaa katika vipute vya Raga ya Dunia na Olimpiki wamekuwa wakiendelea na mazoezi pamoja na kushiriki mapambano mengine muhimu, jambo ambalo timu ya taifa inafaa pia kuanza kufanya.