KIKAPU: Kenya Morans yaanza vibaya kampeni ya kufuzu AfroBasket
2020-11-26 18:33:35| cri

Kenya Morans imeanza vibaya kampeni ya kurejea katika Kombe la Afrika la mpira wa kikapu la wanaume (AfroBasket) baada ya kuwa nje miaka 23 kwa kupepetwa kwa alama 92-54 jijini Kigali nchini Rwanda jana Novemba 25. Washindi wa medali ya fedha ya Afrika kwa mashindano ya wachezaji wanaocheza mpira wa kikapu barani Afrika (AfroCan) Morans waliwapa Wakenya matumaini kuwa wanaweza kuwasumbua ‘simba’ wa Senegal katika robo ya kwanza ambayo ilikuwa nipe-nikupe na kutamatika kwa 19-19. Hata hivyo, vijana wa kocha Cliff Owuor walipoteza mwelekeo katika robo ya pili waliyopoteza 28-14. Morans walijaribu kurejea mechini katika robo ya tatu waliyoshinda 19-11, lakini wakashindwa kabisa kuziba mwanya wa kati ya sita na 10 katika robo hiyo kabla ya kuzidiwa maarifa kabisa katika robo ya mwisho 34-2. Isitoshe, wapinzani wao, ambao waliwabwaga Morans 91-58 katika mechi za makundi na 90-76 katika mechi ya kuamua mshindi wa medali ya shaba katika mashindano ya AfroBasket jijini Nairobi mwaka 1993, walikuwa wazuri sana katika kufunga alama tatu, kupata ikabu na kulinda ngome yao. Mfungaji bora katika mchuano huo wa kufungua mashindano hayo ya Kundi B kwa upande wa Kenya alikuwa Mkenya Tylor Okari anayechezea Bakken Bears nchini Denmark. Okari alipachika alama 13, kumega pasi tano zilizofungwa na kuiba mpira mara mbili. Ibrahima Faye alipachika alama nyingi kwa upande wa Senegal na pia mechi hiyo (19).