Tanzania-Benki ya NMB yazindua kampeni ya Masta Bata kuhamasisha matumizi ya kadi kwenye manunuzi
2020-11-26 16:02:36| cri

 

Benki ya NMB imeanzisha kampeni maalum iitwayo MastaBata inayolenga  kuhamasisha matumizi ya kadi kwenye manunuzi badala ya fedha taslimu.

Manunuzi ya fedha taslimu  yanatajwa kuwa si salama  kwa kuwa  wakati mwengine huchochea  uhalifu.

Uhamasishaji huo wa matumizi ya kadi kwa manunuzi unatajwa kuunga mkono juhudi ambazo pia zinafanywa na serikali,ambayo imeendelea kuboresha mfumo wa malipo mengi kwa kuhakikisha hayafanywi kwa fedha taslimu badala yake yanalipiwa kwa mfumo maalumu ikiwamo kadi na simu za mkononi.

Akizungumza kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi na Menejiment ya NMB,  kwenye  uzinduzi huo jana,Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi, alisema NMB imeamua kutoa fursa ya kipekee kwa wateja wake kufurahia huduma za benki hiyo kupitia promosheni ambayo itatoa zawadi zenye jumla ya Sh. milioni 200.

Kupitia promosheni hiyo itakayoendeshwa kwa miezi mitatu, NMB inalenga kutumia na wateja wake faida waliyoipata, hivyo zawadi mbalimbali zitatolewa, ikiwamo mshindi kuambatana na mwenzi wake kwenda kufanya utalii wa ndani Zanzibar  au kwenye mbuga za wanyama Serengeti na Ngorongoro.