RIADHA: Faith Chepng’etich kuhamia mbio za mita 5,000 baada ya Olimpiki ya Japan
2020-11-27 16:46:11| cri

Bingwa wa Olimpiki katika mbio za mita 1,500, Faith Chepng’etich Kipyegon amefichua azma ya kuanza sasa kunogesha mbio za mita 5,000 baada ya kukamilika kwa Michezo ya Olimpiki ya 2021 jijini Tokyo, Japan. Hata hivyo, bingwa huyo wa zamani wa dunia katika mbio za mita 1,500 amesema hana maazimio ya kushiriki fani mbili tofauti kwa wakati mmoja kama alivyofanya mwanariadha Vivian Cheruiyot aliyetamalaki mbio za mita 5,000 na mita 10,000 kabla ya kuhamia barabarani kwa riadha za masafa marefu. Kipyegon, 26, amejivunia mafanikio tele katika mbio za mita 1,500 – fani ambayo imemzolea dhahabu ya Olimpiki, mataji mengi ya haiba duniani, medali nyingi katika duru za Diamond League, mbio za nyika na mbio za Jumuiya ya Madola mnamo 2014 jijini Glasgow, Scotland. Kipyegon alijivunia mojawapo ya kampeni bora kwenye ulingo wa riadha mwaka huu wa 2020 baada ya kutoshindwa kwenye mashindano matano tofauti huku akisajili muda bora wa dunia wa dakika 1:57.68 kwenye mbio za mita 800 na dakika 2:29.15 katika mbio za mita 1,000 kwenye duru ya Doha Diamond League nchini Qatar.