BoT yaziagiza taasisi za fedha kuweka ulinzi akiba za wateja
2020-11-27 17:01:59| cri

Gavana wa bebki kuu Tanzania amezitaka taasisi za kifedha nchini humo kuwa na kitengo cha kudhibiti vihatarishi ili kuhakikisha wananchi au wateja hawapati hasara na kupoteza akiba zao.

Prof. Florens Lwoga alisema hayo alipokuwa akifungua kongamano la mwaka la siku tatu la Taasisi ya Kudhibiti Vihatarishi Tanzania (IRMT), lililofanyika mjini Bagamoyo mkoani wa Pwani.

Alisema, serikali imeweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha taasisi zote za umma zinakuwa na kitengo cha kudhibiti vihatarishi, kwa kuwa vitengo hivyo vinazuia taasisi au kampuni kupata hasara katika kipindi kigumu ambacho wanapitia au majanga ikiwamo majanga kama ya ugonjwa wa corona.

Kwa upande wake, rais wa IRMT, Pius Maneno, alisema kuna umuhimu wa kila mtu katika jamii  kuwa na tahadhari katika kila kitu anachokifanya kwenye maisha yake hasa biashara. Kwa sababu vitu muhimu vinavyohitajika kuwa na usimamizi wa vihatarishi ni taasisi za kifedha na zile zinazohusiana uwekaji mali kama sekta ya bima.