Rais Xi Jinping wa China atoa Salamu za Mwaka Mpya 2021
2020-12-31 19:47:31| CRI

Rais Xi Jinping wa China atoa Salamu za Mwaka Mpya 202_fororder_1126926048_1609413335703_title0h

Hamjambo! Mwaka wa 2021 unakaribia, ningependa kuwatumia salamu za mwaka mpya kutoka Beijing!

Mwaka 2020 ni mwaka usio wa kawaida. Ili kukabiliana na janga la virusi vya Corona lililoibuka ghafla, tumefafanua upya Upendo kwa Ubinadamu kwa kuzingatia maslahi ya umma na kuthamini maisha ya kila mtu, na pia tumeandika ukurasa mzito wa historia wa kulishinda janga hilo kwa kutegemea mshikamano imara, dhamira thabiti na ustahimilivu mkubwa. Katika kipindi hiki kigumu, tumeshuhudia ushupavu wa kuelekea mahali penye hatari, uhimilivu wa kushikilia majukumu magumu, uwajibikaji wa kupitia dhiki kwa pamoja, na pia tumeshuhudia ushupavu wa kujitoa muhanga na kuguswa na vitendo vya wananchi kujaliana na kusaidiana. Kutoka wahudumu wa afya hadi wanajeshi, kutoka watafiti wa sayansi hadi wafanyakazi wa mitaa, kutoka watu wanaojitolea hadi wafanyakazi wa ujenzi, kutoka wazee hadi vijana, mamia ya maelfu ya watu walitekeleza majukumu yao bila kujali hatari zilizowakabili, na kuwatunza wananchi kwa upendo mkubwa, walikusanya nguvu yao ndogo binafsi kuwa nguvu kubwa ya taifa, na kujenga ukuta imara usiovunjika wa kulinda maisha ya binadamu. kila sura ya mashujaa wasiosita, kila mara wanapopokezana zamu mkono kwa mkono na moyo kwa moyo, kila simulizi linalogusa mioyo yetu, vyote vimeonesha dhamira yetu thabiti ya kulishinda janga hilo. Ukubwa hujengwa kutokana na ukawaida, na mashujaa hujitokeza miongoni mwa wananchi. Kila mmoja wenu ni mkubwa! Ningependa kutoa salamu za pole kwa watu walioambukizwa virusi vya Corona, na kutoa heshima kwa mashujaa wote waliojitokeza kutoka watu wa kawaida! Najionea fahari taifa letu kubwa na wananchi, na pia najionea fahari kutokana na moyo wa taifa letu wa kupigania ustawi bila kusita!

Ushupavu huonekana mbele ya hatari, na dhahabu safi hupatikana baada ya kupitia moto. Kutokana kukabiliana na athari za janga la virusi vya Corona, tumepata mafanikio makubwa katika kuratibu kazi za kuzuia maambukizi na juhudi za kuendeleza uchumi na jamii. Mpango wa 13 wa maendeleo ya Miaka Mitano umekamilika kwa mafanikio, huku Mpango wa 14 ukiwa tayari umeandaliwa. Ujenzi wa Muundo mpya wa maendeleo umeharakishwa, na mpango wa maendeleo yenye ubora wa juu unatekelezwa kwa kina. Nchi yetu imetangulia kutimiza ukuaji chanya miongoni mwa nchi na makundi yenye uchumi mkubwa duniani, na Pato la Ndani la China linatarajiwa kufikia ngazi mpya ya Yuan trilioni 100 kwa mwaka 2020. Uzalishaji wa nafaka umepata mavuno makubwa kwa miaka 17 mfululizo. Vyombo vya utafiti wa kisayansi kwenye anga ya juu na bahari ya kina kirefu kama vile “Tianwen-1”, “Chang’e-5” na “Fendouzhe” vimepiga hatua kubwa. Ujenzi wa bandari ya biashara huria ya mkoa wa Hainan unaendelea hatua kwa hatua. Pia tumefanikiwa kukabiliana na mafuriko makubwa, ambapo wananchi na wanajeshi walishikamana na kushirikiana bila kujali hatari kwenye mapambano dhidi ya maafa hayo, na kujitahidi kupunguza hasara kadiri iwezekanavyo. Nilipofanya ziara za ukaguzi katika mikoa na miji 13, nilifurahia kuona watu wote walikuwa wakifuata kwa makini mwongozo wa kuzuia maambukizi, huku wakijitahidi kurejesha uzalishaji kwa kushindana na wakati, na kufanya juhudi zote kuendeleza uvumbuzi na ubunifu, popote pale nilipotembelea kote nchini, nilihisi moyo wa wananchi wa kujiamini na shauku yao ya kujiendeleza kwa kujitegemea, pia niliona nchi yetu iliyo na ustahimilivu na inayojaa nguvu ya uhai.

Mwaka 2020, tumepata mafanikio makubwa ya kihistoria katika kukamilisha ujenzi wa Jamii yenye maisha bora, na kupata ushindi mkubwa katika vita ya kutokomeza umaskini. Tumeanzisha kampeni kuu dhidi ya ngome ya umaskini uliokithiri, na hatimaye tumefanikiwa kuliondoa tatizo hilo gumu. Baada ya juhudi za miaka minane, watu maskini wapatao milioni 100 vijijini wote wameondokana na umaskini, na wilaya zote 832 maskini kote nchini zimeondolewa kwenye orodha ya maeneo yaliyo nyuma kimaendeleo. Katika miaka hiyo iliyopita, nilitembelea maeneo 14 yaliyokabiliwa na umaskini uliokithiri, dhamira na bidii za wanavijiji wa huko, na michango ya dhati waliyotoa makada wa kupunguza umaskini, mara kwa mara vinaibuka akilini mwangu. Kwa sasa hatutakiwi kusita na bali tunahitaji kuendelea kufanya bidii ili kuimarisha na kupanua mafanikio yaliyopatikana, kujitahidi kutimiza ustawi wa maeneo ya vijijini, na kusonga mbele hatua kwa hatua kuelekea lengo la maendeleo ya pamoja.

Mwaka huu, tumeadhimisha miaka 40 tangu Eneo Maalumu la Kiuchumi la Shenzhen lilipoanzishwa, na miaka 30 tangu eneo la Pudong mjini Shanghai lilipoanza kuendelezwa na kufunguliwa kwa nje. Nilipokuwa kisiwani Hainan na kandoni mwa Mto Huangpu, niliingiwa na hisia nyingi, kwamba maeneo ya majaribio na uvumbuzi yamekuwa mifano ya kuigwa na inayoongoza. Mageuzi na ufunguaji mlango vimetuletea miujiza ya maendeleo, katika siku zijazo tunapaswa kutumia nguvu kubwa zaidi katika kuimarisha mageuzi na kufungua mlango zaidi, ili kuweza kufanikisha zaidi maeneo yaliyotangulia kama hayo.
Njia kuu hufuatwa na wengi, Dunia nzima ni familia moja. Baada ya kupitia yaliyotokea katika mwaka mmoja uliopita, sasa tunaweza kujihisi kwa kina zaidi kuliko wakati wowote ule umuhimu wa Jumuiya ya Binadamu yenye Hatma ya Pamoja. Nilifanya mazungumzo ya simu mara nyingi na marafiki wapya na wa zamani wa kimataifa, na kuhudhuria mikutano kadhaa iliyofanyika kwa njia ya mtandao wa internet, mambo tuliyozungumiza zaidi ni kukuza ushirikiano kwa nia moja, na kushikamana kwenye mapambano dhidi ya virusi vya Corona. Kazi ya kuzuia na kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo bado ni jukumu kubwa na inahitaji juhudi za muda mrefu. Watu wa nchi mbalimbali duniani wanapaswa kushikana mikono na kushirikiana kwa pamoja, ili kuweza kumaliza janga hilo mapema, na kujitahidi kuijenga dunia yetu iwe nzuri zaidi.

Mwaka 2021 ni mwaka wa 100 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Kikomunisti cha China. Katika Safari yetu ya miaka mia moja iliyopita, tumeshuhudia mawimbi na dhoruba, lakini nia yetu ya awali imekuwa ikizidi kuimarika. Kutoka Shikumen mjini Shanghai hadi Ziwa Nanhu mjini Jiaxing, jahazi moja jekundu linalobeba matarajio ya wananchi na matumaini ya taifa, limepita karibu na mwamba mkubwa na kuvuka kwenye mawimbi makali, na hatimaye likawa meli kubwa inayoongoza taifa la China kuelekea kwenye bahari kuu za mbali. Tukiendelea kushikilia mtizamo wa kuzingatia maslahi ya umma, kukumbuka lengo na majukumu yetu ya tangu mwanzoni, tutaendelea na safari zetu za mbali kwa kuvuka mawimbi na dhoruba, na hakika tutaweza kutimiza ustawi mpya wa taifa la China.

Tukisimama kwenye njia panda ya kihistoria kutoka “Miaka 100” ya kwanza kuelekea “Miaka 100” ya pili, safari yetu mpya ya kuijenga China kwa pande zote kuwa nchi ya kisasa ya usoshalisti itaanza. Katika safari hiyo ndefu, tunatakiwa kuendeleza bidii bila kusita. Kutokana na juhudi zetu, tulipitia mambo magumu na tulivuka mabonde na milima. Kwa sasa tunapaswa kuendelea na bidii, na kusonga mbele kwa ushupavu, ili kufikia mafanikio yanayong’ara zaidi.

Wakati huu, usiku umeanza na familia zimejumuika. Mwaka mpya unapokaribia, ninaliombea taifa letu neema na ustawi, na wananchi wetu maisha ya amani na furaha!

Asanteni!