SOKA: Michael Olunga wa Kenya ayoyomea nchini Qatar
2021-01-13 17:59:37| cri

Fowadi Michael Olunga aliamua kuyoyomea nchini Qatar usiku wa Januari 11, 2020 kuchezea kikosi cha Al Duhai SC baada ya kuvunja ndoa na klabu ya Kashiwa Reysol ya Ligi Kuu ya Japan (J1 League). Hatua hiyo ya Olunga inamfanya kuwa Mkenya wa pili baada ya nahodha wa zamani wa Harambee Stars, Dennis ‘The Menace’ Oliech kucheza soka ya kulipwa nchini Qatar. Taifa hilo liliwahi kumpa Oliech ofa ya mamilioni ya pesa ili abadilishe uraia wake na kupata ule wa Qatar. Mbali na kuchezea Nantes, AJ Auxerre na AC Ajaccio za Ufarasa, Oliech aliwahi pia kuchezea Dubai CSC katika Falme za Kiarabu (UAE) kabla ya kutundika rasmi daluga zake akivalia jezi za Gor Mahia mnamo 2019.

Chini ya kocha Sabri Lamouchi ambaye ni raia wa Ufaransa, Al Duhail kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ya vikosi 12. Kikosi hicho kinajivunia alama 27, nane nyuma ya viongozi Al Sadd SC wanaotiwa makali na kiungo mahiri wa zamani wa Barcelona na timu ya taifa ya Uhispania, Xavi Hernandez.