Mdudu wa timua timua anukia Chelsea baada ya matokeo kuzidi kuwa mabaya
2021-01-21 19:11:41| cri

Mambo yanazidi kuwa magumu kwa Kocha Mkuu wa Chelsea, Frank Lampard, na tayari kuna habari kuwa  ya kufutwa kazi kutokana na mwendo mbovu wa timu yake ndani ya Ligi Kuu England. Kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Leicester City, Uwanja wa King Power kinawashusha kwa nafasi moja kutoka ile ya 7 mpaka ya 8 ikiwa na pointi zake 29 baada ya kucheza mechi 19. Leicester City walipata ushindi na kubeba pointi tatu baada ya Wilfred Ndidi kupachika bao katika dakika ya 6 na James Maddison kupachika bao dakika ya 41. Ikiwa imecheza mechi tatu za Ligi Kuu England katika mwezi huu, Chelsea imeshinda mchezo mmoja dhidi ya Fulham ambapo ilishinda bao 1-0, lakini ilikuwa ni bahati ya Fulham kuwa pungufu baada ya mchezaji mmoja kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 44, kabla ya hapo ilichapwa mabao 3-1 dhidi ya Manchester. Aliyekuwa kocha wa Paris Saint Germain Thomas Tuchel ni mmoja wa watu makocha anayepigiwa upatu kuchukua nafasi ya Frank, lakini mbali na Tuchel pia yuko Max Allegr wa Italia ambaye sasa hana timu, na Ralph Hasenhüttl ambaye amefanya vizuri kwenye klabu ya Southampton.