Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Wanaotafuta Uhuru wa Kiuchumi
2021-01-25 20:01:28| CRI

Gazeti la China Youth Daily hivi karibuni limewahoji wanafunzi 808 wa vyuo vikuu kuhusu maoni yao juu ya uhuru wa kiuchumi, na uchunguzi huo unaonesha kuwa asilimia 89.32 ya waliohojiwa wanatafuta uhuru wa kujitegemea kiuchumi, na asilimia 72.88 kati yao wameanza hatua na kutimiza viwango tofauti vya uhuru wa kiuchumi, huku asilimia 8 wakitimiza lengo hilo kikamilifu.

Tofauti na vizazi vilivyopita, kuzipunguzia mizigo familia zao hakukuwa tena lengo kuu la wanafunzi hao kutafuta uhuru wa kiuchumi. Wanachotarajia ni kutumia pesa walizopata kwa kujitegemea, ili kujisikia uhuru, kujivunia na moyo wa kuwajibika kijamii. Wanafunzi wengi waliohojiwa wamesema kutimiza uhuru wa kiuchumi kumewaletea furaha kubwa.

Uchunguzi unaonesha kuwa “uhuru wa kiuchumi ni jambo poa”, “kuna baadhi ya matumizi ya pesa ambayo hawataki kuwaambia wazazi”, sababu hizi mbili zinachukua asilimia 46.87 na asilimia 47.15 mtawalia, ikifuatiwa na sababu kubwa ya tatu ambayo ni “Wamekuwa watu wazima, na hivyo hawataki tena kuomba pesa kwa wazazi”.

Takwimu zinaonesha kuwa miongoni mwa wanafunzi 805 waliohojiwa, asilimia 8.1 wametimiza uhuru kamili wa kiuchumi, asilimia 11.54 wanachangia nusu ya matumizi yao, na asilimia 54.24 ya waliohojiwa wanaona mbali na pesa wanazopewa na wazazi, pia wana vyanzo vingine vidogo vya kiuchumi.