Idadi ya watumiaji wa Internet nchini China yakaribia bilioni moja
2021-02-09 16:49:58| cri

Ripoti ya 47 kuhusu maendeleo ya mtandao wa Internet nchini China iliyotolewa Februari 3 na Kituo cha Taarifa za Internet cha China CNNIC inaonesha kuwa hadi kufikia mwezi Desemba mwaka 2020, idadi ya watumiaji wa Internet nchini China imefikia milioni 989, ikiwa ni asilimia 70.4 ya jumla ya watu wa China. Bado kuna watu milioni 416 wasiotumia mtandao wa Internet, ambapo wengi wao wako kwenye maeneo ya vijijini au ni wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 60.

Takwimu zilizotolewa kwenye ripoti hiyo zinaonesha kuwa kwenye kipindi cha janga la COVID-19, jumla ya watu milioni 900 walijiandikisha kupata kitambulisho cha kidijitali kuhusu hali ya afya“Health QR Code”, ambacho kwa ujumla kimetumika mara bilioni 40, na kimetoa mchango mkubwa katika juhudi za kudhibiti janga hilo na kufungua tena uchumi baada ya janga.

Takwimu zinaonesha kuwa mpaka kufikia mwezi Desemba mwaka jana, idadi ya watumiaji wa huduma za elimu na afya za mtandaoni imefikia milioni 342 na milioni 215 mtawalia, ikiwa ni asilimia 34.6 na asilimia 21.7 ya jumla ya wanamtandao nchini China.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watumiaji wa Internet milioni 309 wako kwenye maeneo ya vijijini, ambako asilimia 55.9 ya wakazi wanatumia mtandao huo, ikiwa ni ongezeko la asilimia 9.7 kuliko mwezi Machi mwaka jana.