RIADHA: Kipchoge kwenda Ujerumani kujiandaa na mashindano ya Hamburg Marathon
2021-02-19 17:00:33| CRI

Mshikizi wa rekodi ya dunia katika mbio za kilomita 42, Eliud Kipchoge raia wa Kenya, ametangaza atarejea mjini Hamburg nchini Ujerumani Aprili 11. Kupitia mitandao yake ya kijamii, bingwa huyo wa Olimpiki na mshikilizi wa rekodi ya dunia ya umbali huo ya saa 2:01:39 alisema kuwa atarejea katika mji huo alikoanzia utimkaji wa mbio za kilomita 42 mwaka 2013. Kipchoge alifichua mpango huo wake saa chache baada ya timu yake ya NN Running pia kuthibitisha kuwa mkimbiaji huyo mwenye umri wa miaka 36 atakuwa katika orodha ya zaidi ya watimkaji nyota 100 watakaowania ubingwa wa Hamburg Marathon. Timu hiyo ilitangaza ushirikiano na waandalizi wa Hamburg Marathon juma lililopita kuandaa mbio hizo katika eneo ambalo washiriki pekee wataruhusiwa.