Sudan Kusini yafikiria kurefusha hatua kiasi za zuio kutokana na kuongezeka kwa maambukizi ya COVID-19
2021-03-01 09:09:38| CRI

Maofisa wa wizara ya afya ya Sudan Kusini wamesema wanapanga kurefusha kwa mwezi mmoja zaidi hatua kiasi za zuio zilizowekwa hivi karibuni kutokana na ongezeko la maambukizi ya COVID-19.

Ofisa mwandamizi katika wizara ya afya ya Sudan Kusini Bw. Richard Lako, amesema hatua hiyo inatokana na maambukizi ya COVID-19 kuongezeka na kufikia 7,926 na idadi ya vifo kufikia 93 hadi kufikia jana Jumapili.

Bw. Lako amewaambia wanahabari mjini Juba kuwa kuna maambukizi kwenye jamii na idadi ya maambukizi inazidi kuongezeka, hivyo ametoa mwito wa kurefusha vizuizi kiasi vilivyopo ili kupunguza maambukizi. Kwa sasa maambukizi yanagunduliwa zaidi miongoni mwa wasafiri.

Bw. Lako ameongeza kuwa serikali itaanza kuwazuia watu wasio na barakoa kutoka nje, ikiwa ni hatua ya kuimarisha hatua za afya, na pia ameonya kuwa serikali inaweza kuanza kuwakamata na kuwashitaki watu wanaokiuka hatua hizo.