Rais wa Kenya aahidi kuimarisha umoja wa kikanda anapokuwa mwenyekiti wa jumuiya ya Afrika Mashariki
2021-03-01 09:10:11| CRI

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ameahidi kuhimiza umoja na maendeleo ya jumuiya ya Afrika Mashariki wakati kiongozi huyo anachukua nafasi ya mwenyekiti wa jumuiya hiyo.

Akihutubia mkutano wa 21 wa kawaida wa wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika kwa njia ya video, Rais Kenyatta amesema ataweka mkazo katika kukuza ushirikiano ili kuimarisha muunganiko wa jumuiya ya Afrika Mashariki, na kuhakikisha utekelezaji endelevu wa miradi na programu kwenye sekta zenye tija.

Rais Kenyatta ameahidi kuwa ataiendeleza jumuiya ya Afrika Mashariki, na kufanya kila juhudi kuhimiza kufikiwa kwa malengo ya pamoja yaliyofanya jumuiya hiyo kufufuliwa miaka 20 iliyopita.

Kwenye mkutano huo wa kilele Bw. Peter Mutuku Mathuki aliapishwa kuwa katibu mkuu mpya wa jumuiya ya Afrika Mashariki kwa muhula wa miaka mitano kuanzia Aprili 25, akichukua nafasi hiyo kutoka wa Bw. Liberat Mfumukeko ambaye anamaliza muda wake.