Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja, ametoa wito kwa watanzania kuweka utaratibu wa kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini na kuacha kuamini vivutio ni kwa ajili ya wageni kutoka nje.
Wito huo umetolewa leo Alhamisi Februari 25, kwenye kikao cha pili cha bodi ya barabara mkoa wa Mwanza kwa mwaka wa fedha 2020/2021 kilichofanyika jijini Mwanza ambapo amesisitiza ni vvema kila mtu ahamasike kutembelea vivutio vya utalii ikiwemo mbuga za wanyama na hifadhi za taifa.
Amesema Watanzania wanapaswa kuwa wazalendo kwa kupenda vivutio vyao na kuvitangaza kwani kuanzia mwaka 1993 kulikuwa na watalii waliokuwa wakiingia kwenye hifadhi 230,000 na hadi kufikia mwaka 2019 idadi ya watalii iliongezeka na kufikia milioni 1.5 waliofanya utalii kwenye mbuga mbalimbali zilizopo nchini humo.