Kenya: Wito mserikali isiingize taifa kwenye madeni zaidi
2021-03-01 18:42:31| cri

Muungano wa wadau katika masuala ya uchumi na biashara wametoa wito kwa wizara ya Fedha itilie maanani hali ya sasa ya kiuchumi inapotayarisha makadirio ya bajeti ya mwaka huu wa kifedha kuepusha Kenya isizame zaidi katika lindi la madeni.

Washika dau hao wakiongozwa na Mbunge wa Kiambu Mjini Bw Jude Njomo, walisema ipo haja ya kuzindua utaratibu wa kuandaa bajeti kwa lengo la kuimarisha nidhamu katika udhibiti wa kuongezeka kwa deni la kitaifa.

Bw Njomo alisema hayo wakati wa mkutano uliojumuisha Kamati ya Bajeti ya Bunge, Taasisi ya Umma kuhusu utafiti na mwongozo (KIPPRA), Tume ya Ugavi wa Rasilmali (CRA), Jumuiya ya kuokoa Uchumi na Wadau wa Ushauri wa Westminster mjini Mombasa.

Washiriki hao walisema Wizara ya Fedha na Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA), zapasa kuelewa na changamoto zinazokumba wananchi ndipo zisiwasilishe bajeti itakayoumiza walipa kodi na kupelekea serikali kukopa pesa zaidi kugharimia shughuli za maendeleo.

Hata hivyo, mwenyekiti huyu wa kamati ya Bunge kuhusu bajeti alisema lazima mikakati izinduliwe kuhakikisha wanaotekeleza mwongozo kusimamia ukopaji wa madeni wamefuata utaratibu uliowekwa.

Kufuatia kuwasilishwa kwa mwongozo wa maandalizi ya Bajeti na Taarifa ya Kimikakati kuhusu masuala ya bajeti ya 2021 bungeni wiki moja iliyopita , Bw Njomo alisema wakati umewadia wa kuimarisha nidhamu katika udhibiti wa madeni.

Muungano huu wa washika dau katika masuala ya kiuchumi hujumuisha wabunge pamoja na watalaam wengine waliobobea katika masuala ya kiuchumi.

Baada ya kupata idhini ya Spika wa bunge la kataifia, muungano huu wa washika dau hukongamana kubuni miongozo na kuelekeza majadiliano bungeni.

Washiriki katika kongamano hilo lililofanyiwa mjini Mombasa waliitaka wizara ya fedha itilie maanani athari za janga Covid-19 kwa wananchi inapoibua taratibu za ufufuzi wa uchumi.