Kijana mwenye ugonjwa sugu wa misuli agundua nyota sita baada ya kuangalia picha laki tatu za anga za juu
2021-03-01 15:45:29| cri

Hivi karibuni kijana mmoja kutoka mkoa wa Hubei, China mwenye ugonjwa sugu wa misuli amepata umaarufu kwenye mitandao ya kijamii.

Habari zinasema, kijana huyo aliyezaliwa mwaka 1997 amesumbuliwa na tatizo sugu la upungufu wa nguvu za misuli tangu utotoni, na pia vigumu kwake kuongea, kutembea na kuandika, na kila siku anatakiwa kutumia dawa nyingi ili kudhibiti ugonjwa huo.

Lakini kutokana na upendo wake kwa hisabati na unajimu, kijana huyo anayejulikana kwa jina la Zhao Jingyuan, alitumia miaka mitano kuangalia picha zaidi ya laki tatu za anga za juu, na kufanikiwa kugundua nyota sita, zikiwemo Super Nova nne na nyota mbili zilizo nje ya Galaxy yetu, kati yao, nyota moja iko umbali wa miaka-nuru (Light year) milioni 250 kutoka Dunia. Kijana Zhao amesema angependa kutumia maisha yake yote kutafiti anga za juu.

Kituo cha Unajimu cha Xingming na Kituo cha Unajimu cha mtandaoni cha China-VO vimemwajiri Bw. Zhao kuwa “naibu mkurugenzi wa sekritarieti”, hatua ambayo imetambua uwezo wake wa kitaaluma.

Mwanamtandao mmoja wa China ametoa ujumbe kwamba kijana Zhao ana nia thabiti inayoushinda ugonjwa sugu unaomsumbua, na watu wenye ndoto kama yeye ndio wanaostahili kusifiwa!