Serengeti yatangazwa mbuga bora zaidi duniani
2021-03-04 19:07:48| cri

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, imeshinda tuzo ya kuwa mbuga bora zaidi ya hifadhi ya wanyama duniani.

Hayo yalisemwa jana mjini Morogoro na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbalo wakati wa maadhimisho ya siku ya wanyamapori duniani yaliyokwenda sambamba na mkutano wa wadau wa sekta ya utalii.

Akizungumza katika hafla hiyo Dk. Ndumbalo alisema Tanzania imeshinda tuzo hiyo na kuwa ya kwanza kupitia hifadhi ya Taifa ya Serengeti, huku Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Mlima Kilimanjaro zikiwa zimeshika nafasi za juu katika tuzo hizo ambazo hutolewa na Chief Traveler Award (CTA).

Dk. Ndumbalo alisema kuwa mafaniko hayo hayakuja tu bali yametokana na mikakati ya dhati ya serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli katika uwekezaji na usimamizi madhubuti ya hifadhi za Taifa.