Uzoefu wa China wa kuondokana na umaskini umetoa mfano mzuri wa kuigwa kwa nchi za Afrika
2021-04-07 18:06:25| Cri

Ofisi ya Habari katika Baraza la Serikali la China imetoa Waraka kuhusu Uzoefu wa China katika kupunguza umaskini ambao umesifiwa na wataalamu wa nchi mbalimbali. Wataalam hao wanaona kuwa chini ya uongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China CPC, kazi ya kuondokana na umaskini nchini China imepata mafanikio ya kihistoria, na kutoa mchango mkubwa kwa ajili ya kazi ya kupunguza umaskini duniani na maendeleo ya binadamu, na uzoefu huo mzuri wa China unastahili kuigwa.

Mtafiti wa Kituo cha utafiti wa mawasiliano ya uchumi na utamaduni kati ya China na Afrika kutoka nchini Zimbabwe, Bw. Donald Rushambwa alisomea shahada ya uzamili nchini China tangu mwaka 2014 hadi 2019, na kufanya utafiti katika mikoa ya Zhejiang, Jiangsu, Gansu na Liaoning, ambapo alishuhudia mafanikio makubwa yaliyopatikana na China katika kupunguza umaskini. Anasema:“China imepata mafanikio makubwa katika kuondokana na umaskini. Hali iliyoniwekea kumbukumbu zaidi ni kuwa, katika sehemu ya vijijini, serikali iliwahimiza wanakijiji kutafuta kazi mijini, ili kupata utajiri, wakati huo huo serikali pia ilitoa fursa nyingi za nafasi za ajira vijijini, kama vile walinzi wa misitu, hatua ambayo imetatua suala la ajira, huku ikilinda mazingira, na kuboreshwa kwa mazingira pia kutasaidia utekelezaji wa kazi ya kupunguza umaskini.”

Bw. Rushambwa ameeleza kuwa, kazi ya kupunguza umaskini ya China ni mfano mzuri wa kuigwa na Zimbabwe, na kwamba Zimbabwe inatakiwa kujifunza kwa China, kutumia sifa ya raslimali za watu, kuongeza bajeti katika mambo ya kilimo na elimu, ili kutimiza lengo la kuondoa umaskini. Anasema:“Naona kuwa nchi zinazoendelea duniani ikiwemo Zimbabwe zina maliasili nyingi haswa raslimali za watu, lakini hazijatumiwa vya kutosha. Rais Xi aliwahi kusema kuondoa umaskini kunapaswa kutimizwa kwa kutegemea juhudi za watu maskini. Mimi pia nakubali, kwani tunahitaji kuondokana na umaskini kwa juhudi za pamoja.”

Vilevile Bw. Rushambwa ameisifu China kwa kutoa mapendekezo kwa nchi za Afrika kuondokana na umaskini, akisema China inazisaidia nchi za Afrika katika ujenzi wa miundo mbinu, na kufanya ushirikiano wa biashara na nchi za Afrika. China ikiwa mwenzi mkubwa zaidi wa biashara wa Afrika, imehimiza maendeleo ya uchumi na jamii na pia kuhimiza maendeleo ya uhusiano kati ya pande hizo mbili.