Msichana wa Nanjing aanzisha duka la mtandaoni la kuuza hadithi
2021-04-07 15:41:40| Cri

Kwenye duka moja la mtandaoni linaloitwa “CY Stories”, unaweza kutumia yuan moja kununua hadithi moja ya kweli yenye furaha na upendo, inayoweza kugusa moyo wako.

 

Hidithi zote hizo zilikusanywa kutoka kwa watu wa kawaida wasiojulikana. Hadithi ya kwanza iliyoko kwenye duka hilo ni kwamba babu anayefanya kazi katika mji mwingine, alimtumia bibi chupa moja ya manukato, lakini Bibi hakujua ni kitu gani, kwa hivyo alitia manukato yote kwenye chai na kuwafanya jamaa wote wanywe kidogo.Hadithi hiyo iliwekwa kwenye duka hilo siku ya kwanza lilipoanzishwa rasmi mwaka 2012.

Mwenye duka Cong Pingping ni mwandishi, lengo lake la awali ni kukusanya hadithi na kutafuta hamasa kwa ajili ya kazi yake.

Bi. Cong Pingping alisema mwanzoni alitoa tu hadithi alizozikusanya katika miaka mingi kwenye duka hilo, anatumai kuwa wasomaji watatoa hadithi zao wenyewe kama wakiwa na uzoefu au hadithi zinazofanana.  

Siku hadi siku duka hilo limetembelewa na kufuatiliwa na watu wengi zaidi, na hadithi ya 191 inayohusu upendo wa familia imeuzwa mara zaidi ya elfu tisa, ikiwa ni moja ya hadithi zinazopendwa zaidi na wasomaji katika duka hilo.

Katika miaka tisa iliyopita tangu lilipoanzishwa, duka hilo limefuatiliwa na wanamtandao zaidi ya laki tatu, na kwa ujumla limekusanya hadithi mbalimbali za kweli zaidi ya elfu mbili.

Cong Pingping alisema, baadhi ya wasomaji walitia shaka kwamba hadithi nyingi ni za kawaida sana, lakini anaona kila hadithi ni sehemu muhimu ya maisha ya msimulizi wake, kwa hivyo inastahili kuhifadhiwa ipasavyo.