Rais Xi Jinping wa China ahutubia ufunguzi wa mkutano wa Baraza la Boao
2021-04-20 17:27:17| CRI

Rais Xi Jinping wa China ahutubia ufunguzi wa mkutano wa Baraza la Boao_fororder_2021042011453662974

Mkutano wa mwaka 2021 wa Baraza la Asia la Boao umefunguliwa leo asubuhi huko Boao mkoani Hainan. Rais Xi Jinping wa China amehutubia ufunguzi huo kwa njia ya video, akipendekeza nchi mbalimbali barani Asia na duniani zishirikiane kukabiliana na janga la COVID-19, kuimarisha usimamizi wa mambo ya kimataifa, kujenga “Ukanda Mmoja, Njia Mmoja” kwa pamoja, na kusukuma mbele ujenzi wa jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja.

Rais Xi amefafanua mapendekezo yake katika pande nne, ikiwa ni pamoja na kufanya mazungumzo yenye usawa, ili kuanzisha mustakabali wenye mafanikio ya pamoja, kufungua mlango na kufanya uvumbuzi, ili kuanzisha mustakabali wenye maendeleo na ustawi, kushikamana na kushirikiana, ili kuanzisha mustakabali wa afya na usalama, na kushikilia haki, ili kuanzisha mustakabali wenye kuheshimiana na kupeana mafunzo.

Rais Xi amesema inapaswa kulinda mfumo wa kimataifa ambao kiini chake ni Umoja wa Mataifa, utaratibu wa kimataifa ambao kiini chake ni sheria za kimataifa, na mfumo wa biashara ya kimataifa ambao kiini chake ni Shirika la Biashara Duniani. Anasema, “Mambo ya kimataifa yanatakiwa kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo, na hatma ya dunia inapaswa kudhibitiwa kwa pamoja na nchi zote duniani. Badala ya umwamba, dunia inahitaji haki. Nchi kubwa lazima iwe nchi kubwa inawajibika, ambayo inahitaji kubeba majukumu zaidi.”

Kuhusu ujenzi wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” Rais Xi amesisitiza kuwa China inakaribisha nchi yoyote duniani kushiriki kwenye ujenzi huo, ili kupata manufaa ya pamoja. Anasema, “Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Benki ya Dunia, hadi kufikia mwaka 2030, ujenzi wa ‘Ukanda Mmoja, Njia Moja’ utasaidia watu milioni 7.6 kuondokana na umaskini uliokithiri, na watu milioni 32 kuondokana na umaskini wa kiwango cha katikati. Tutafuata moyo wa kushirikisha, na kufanya juhudi pamoja na pande zote husika, ili kupunguza umaskini na kuhimiza maendeleo kupitia ‘Ukanda Mmoja, Njia Moja’, na kuchangia ustawi wa pamoja wa bindamu.”

Rais Xi amesisitiza kuwa bila kujali China itapata maendeleo ya kiasi gani, daima haitafanya umwamba, haitavamia nchi nyingine, haitajaribu kudhibiti kanda fulani, na haitapimana nguvu ya kijeshi na nchi nyingine. Aidha China itashiriki kwenye ushirikiano wa pande nyingi za biashara na uwekezaji kwa hatua madhubuti, na kukaribisha nchi za nje kunufaika na soko kubwa la China.