Klabu ya Schalke 04 ya ujerumani yashuka daraja baada ya miaka 30 Bundesliga
2021-04-22 17:41:10| cri

Schalke 04, ambayo iko mkiani wa Ligi Kuu ya soka Ujerumani, jana Jumanne ilishuka daraja baada ya kucheza Bundesliga kwa misimu 30 mfululizo na karibu miaka kumi baada ya kufika nusu fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kipigo cha bao 1-0 ilichopewa na Arminia Bielefeld kilihitimisha kushuka daraja kwa mara ya nne katika historia ya Schalke. Schalke ilicheza dakika 19 za mwisho ikiwa pungufu ya mchezaji mmoja baada ya beki Malick Thiaw kuonyeshwa kadi ya pili ya njano. Nahodha wa Bielefeld, Fabian Klos alifunga bao hilo la ushindi mapema katika kipindi cha pili na kuilazimisha Schalke kushuka daraja kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1988.