Somalia yakaribisha pendekezo la Umoja wa Afrika kuhusu uchaguzi huru na wa haki
2021-04-23 09:05:42| CRI

Somalia imekaribisha pendekezo la Umoja wa Afrika kufanikisha mazungumzo ya kiujenzi kati ya viongozi wa kisiasa wanaovutana, yatakayosaidia kufanyika kwa uchaguzi huru, wa haki na ulio wazi kwa mujibu wa katiba ya Somalia.

Waziri wa habari wa Somalia Bw. Osman Dubbe amepongeza juhudi za Baraza la amani na usalama la Umoja wa Afrika (AUPSC) lililokutana jana kujadili namna ya kuisaidia Somalia kuondoa mkwamo wa kisiasa na kutandika njia ya uchaguzi.

Hata hivyo Bw. Dubbe amezilaumu Kenya na Djibouti kwa kampeni yao ya kuyumbisha mchakato wa kisiasa nchini Somalia, kwa kujaribu kushawishi matokeo ya mkutano wa jana. Amesema serikali ya Somalia inajua uingiliaji wa Kenya na Djibouti kwenye juhudi zinazoendelea za Umoja wa Afrika kujaribu kuwawezesha wasomali kujiamulia mambo yao.