Anglogold Ashanti, Tanzania zakubaliana kuendeleza ushirikiano
2021-04-23 18:39:34| cri

Kampuni ya Madini ya Anglogold Ashanti ya Afrika Kusini imeahidi kuendeleza ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika sekta ya madini na kuhakikisha kuwa sekta hiyo iko imara katika kukuza uchumi wa nchi hiyo.

Ahadi hiyo imetolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Anglogold Ashanti – Afrika, Sicelo Ntuli wakati alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Balozi Liberata Mulamula mjini Dar es Salaam.

Akiongea mara baada ya mazungumzo hayo Balozi Mulamula amesema kuwa, Anglogold Ashanti ni wadau wakubwa katika sekta ya madini na wameonesha utayari wao wa kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kukuza na kuendeleza sekta ya madini.  Balozi Mulamula ameongeza kuwa kitendo cha kukutana na wadau wa madini kama Anglogold Ashanti na kujadiliana nao masuala mbalimbali ya ushirikiano wa kukuza sekta ya madini ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya Diplomasia ya Uchumi. Kampuni ya Anglogold Ashanti iliingia ubia na Kampuni ya BG Umoja ya nchini Tanzania kwa ajili ya kuchimba madini katika miradi ya Nyankanga na Geita Hill. Anglogold ni Kampuni mama ya Geita Gold Mine (GGML) imeipatia BG Umoja mkataba wenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 186 kwa miaka miwili.