Mashabiki Wa Schalke wawashambulia wachezaji kwa mayai baada ya kushuka daraja
2021-04-23 16:40:37| cri

Wachezaji wa Schalke pamoja na maofisa wao wa benchi la ufundi walishambuliwa na mashabiki wao waliowarushia mayai baada ya kikosi hicho kushushwa daraja kwenye Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa mara ya kwanza baada ya miaka 33. Schalke wameshushwa daraja msimu huu baada ya kichapo cha 1-0 kutoka kwa Arminia Bielefeld. Mechi hiyo ilikuwa yao ya 21 kupoteza kwenye kampeni za muhula huu. Mnamo Jumatano, zaidi ya mashabiki 600 waliingia katika uwanja wa Schalke Stadium na kuwavamia wachezaji pamoja na vinara wa kikosi hicho huku wakiwazomea na kuwarushia mayai. Kabla ya kufanikiwa kuingia uwanjani mashabiki hao ambao sehemu kubwa walitiwa nguvuni na maafisa wa polisi mjini Gelsenkirchen, walikua wamewasha moto mkubwa nje ya uwanja huku wakifyatua fataki.