Wakulima wa miwa Uganda wataka bunge kuwasaidia ili miwa yao inunuliwe
2021-04-23 18:39:13| cri

Wakulima wa miwa katika wilaya ya Luuka nchini Uganda wamelazimika kusalia na miwa yao baada ya kampuni za sukari kukataa kuinunua kwa kipindi cha miezi nane sasa. Wakulima hao 300 walikuwa wamefanya makubaliano na kampuni za sukari nchini humo zikiwemo kampuni za sukari za Mayuge na Madhvani kuwakuzia miwa lakini kampuni hizo hadi sasa zimekataa kununua miwa yao ambayo wanadai huenda ikaharibikia shambani. Jumatano wiki hii, wakulima hao walipeleka malalamiko yao bungeni wakimtaka spika wa bunge la Uganda Rebecca Kadaga kuingilia kati suala hilo ili kampuni hizo za sukari zinunue miwa yao. Wakulima hao wamesema hivi sasa wanapitia kipindi kigumu kwa kuwa wameshindwa hata kulipia wanao karo ya shule pamoja na chakula majumbani mwao. Wameongeza kuwa mali zao huenda zikachukuliwa na benki baada ya kushindwa kulipa mikopo waliochukua kwa ajili ya upandaji wa miwa.