Waliochanjwa Chanjo ya Corona Marekani Wazawadiwa Bangi ya Bure
2021-04-27 16:06:18| Cri

Huku kukiwa na utata kuhusu chanjo ya virusi vya corona ulimwenguni kutokana na madhara yake, kuna baadhi ya mataifa ambayo yanatumia mbinu mbadala kuhakikisha wananchi wanachanjwa. Kwa mfano wakazi wa jimbo la New York nchini Marekani ambao wamekuwa wakipokea chanjo ya Covid-19, wamekuwa wakipongezwa kwa kuzawadiwa msokoto wa bangi.

Hii ni baada ya matumizi ya bangi kuidhinishwa kisheria jimboni humo na serikali. Katika njia ya kusherehekea, wanaharakati siku ya Jumanne, Aprili 20, walikuwa wakimpatia mtu yeyote mjini Manhattan msokoto wa bangi baada ya kuthibitisha amepokea chanjo hiyo. Kulingana na mmoja wa waandaaji wa shughuli hiyo Michael O’Malley, hatua hiyo ni njia ya kuunga mkono zoezi la kutoa chanjo ya corona.

Michael pia alisema wanajaribu kuhamasisha umma ili wahalalishe kisheria matumizi ya mmea wa bangi katika taifa nzima la Marekani. “Hii ni mara ya kwanza tunaweza kuketi pamoja na kuwapatia kisheria watu bangi. Tunaunga mkono juhudi za shirikisho za utoaji wa chanjo. Na pia tunajaribu kuhamasisha wahalalishe kisheria matumizi ya mmea wa bangi katika nchi nzima ,” Michael aliliambia shirika la habari la AFP.