Rais wa Uganda awataka marais wenzake kuungana ili kuimarisha usalama na kuhimiza maendeleo
2021-05-14 09:17:39| CRI

Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye ameapishwa kuwa Rais wa Uganda kwa kipindi kingine cha miaka mitano, amewataka marais wenzake wa nchi za Afrika kuwa na umoja ili kuhakikisha usalama na maendeleo ya bara la Afrika.

Akihutubia kwenye sherehe ya kuapishwa kwake, Rais Museveni amewaambia marais 11 waliohudhuria sherehe hiyo kuwa Afrika inatakiwa kutafuta nafasi yake kwenye jukwaa la kimataifa.

Rais Museveni amesema maendeleo ya Afrika yamekwama kwa muda mrefu kutokana na kukosekana kwa umoja na uingiliaji wa mataifa ya kigeni. Amesema ili Afrika iweze kujihakikishia usalama wake wa kimkakati, inatakiwa kuwa na mafungamano ya kiuchumi, na kuwa na aina fulani ya shirikisho la kisiasa.

Amesema anafurahia kuona nchi za Afrika zinafanya kazi kuelekea kwenye Eneo la biashara huria la Afrika, na kwenye shirikisho la kisiasa la nchi za Afrika Mashariki.