Serikali ya Kenya yasema shirika la Marekani lapanga kukwepa ushuru
2021-05-14 17:07:42| cri

Waziri wa Afya wa Kenya Bw Mutahi Kagwe amesema kuwa Shirika la Amerika la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) lilikuwa likijaribu kukwepa kulipa ushuru katika uingizaji za dawa za kukabili makali ya virusi vya HIV. Taarifa hii inakuja wakati ambapo kumekuwa na mvutano mkali kati ya serikali na shirika hilo kuhusu uingizaji wa dawa hizo nchini, ambazo zimekuwa zikizuiliwa katika Bandari ya Mombasa tangu Januari.

Licha ya serikali kutangaza kuondoa hitaji la shirika kulipa Sh45 milioni kama ushuru, ahadi hiyo haijatekelezwa. Bw Kagwe alisema kuwa baada ya kubaini hayo, serikali imeanza kuweka masharti makali kuhakikisha kuwa mashirika ya misaada yanayohudumu nchini yanaendesha shughuli zake kwa uwazi.

Mashirika mengi ya kutetea watu wanaoishi na virusi vya ukiwmi yanasema utata huo unaendelea kuhatarisha maisha ya zaidi ya Wakenya 1.2 milioni ambao hutegemea dawa hizo kupunguza makali ya virusi hivyo.Huku serikali ikishikilia kuwa shirika hilo lilitumia njia za “kijanja” kuingiza dawa nchini Kenya, shirika hilo nalo linashikilia kuwa halitakubali dawa hizo zisambazwe nchini Kenya na Halmashauri ya Kusambaza Dawa Kenya (Kemsa) kutokana na tuhuma za ufisadi zinazoikabili.

Kemsa imejipata katika utata baada ya mabilioni ya pesa kupotea katika hali tatanishi kwenye utoaji kandarasi za ununuzi wa vifaa vya kuisaidia Kenya kukabili virusi vya corona mwaka uliopita.