Reli ya kwanza ya SGR iliyojengwa na kampuni ya China katika Afrika Magharibi yaanza safari za kibiashara
2021-06-16 07:53:47| CRI

Juni 10, Reli kati ya Lagos na Ibadan nchini Nigeria ambayo ni mradi mkubwa wa ushirikiano wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” kati ya China na Afrika uliojengwa na kampuni ya ujenzi na uhandisi ya China CCECC, imeanza rasmi safari za kibiashara, ikiwa ni reli ya kwanza ya SGR yenye njia mbili katika kanda ya Afrika Magharibi.

Hafla ya uzinduzi wa reli hiyo ilifanyika Alhamis iliyopita mjini Lagos, na kuhudhuriwa na Rais wa nchi hiyo, Muhammadu Buhari, spika wa baraza la wawakilishi la Nigeria Femi Gbajabiamila, balozi wa China nchini Nigeria Cui Jianchun, waziri wa uchukuzi Rotimi Amaechi na maofisa wengine wa serikali ya nchi hiyo.

Reli hiyo inayounganisha jiji la Lagos ambalo ni mji mkubwa zaidi barani Afrika, na Ibadan ambao ni mji muhimu wa viwanda ulioko kusini mwa Nigeria, ilianza kujengwa mwezi Machi mwaka 2017, na kuanza safari za majaribio mwezi Desemba mwaka 2020. Reli hiyo ya SGR yenye urefu wa kilomita 157 na mwendo wa kilomita 150 kwa saa, ilijengwa kwa ufadhili wa Benki ya Exim ya China. Kuanza kwa safari katika reli hiyo kutaboresha kidhahiri mazingira ya usafiri kwenye sehemu ya kusini ya Nigeria, kurahisisha usafiri kwa wakazi wa huko, na pia kutaunganisha maeneo ya ndani na bandari, na hivyo kutoa mchango mkubwa katika kuharakisha usafirishaji wa bidhaa zinazoingia na kutoka nchini humo, na kuhimiza maendeleo ya uchumi hasa katika maeneo yaliyoko karibu na reli hiyo.

Katika hafla hiyo Rais Buhari alisema, kukamilika kwa ujenzi wa reli ya Lagos-Ibadan, ikiwa ni sehemu ya mradi wa kuifanya sekta ya reli ya nchi hiyo iwe ya kisasa, ni hatua nyingine muhimu iliyofikiwa kwenye juhudi za serikali ya Nigeria za kustawisha miundombinu. Anasema,

“Kuanza safari za reli kati ya Lagos na Ibadan kuna umuhimu mkubwa, kwa kuwa imejenga ushoroba wa uchukuzi wa mizigo wa moja kwa moja kati ya miji hiyo miwili. Mizigo itaweza kusafirishwa moja kwa moja kutoka bandari ya Apapa mjini Lagos kwa njia ya reli kwenda kwenye bandari kavu ya mjini Ibadan, na kisha kusambazwa kwenye maeneo mengine ya Nigeria.”

Reli ya Lagos-Ibadan, ikiwa ni mradi mkubwa wa ushirikiano wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” na sehemu muhimu ya mtandao wa reli wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), itasukuma mbele ujenzi wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” katika kanda ya Afrika Magharibi, na kuhimiza maendeleo ya uchumi na jamii nchini Nigeria, na vilevile mawasiliano ya kiutamaduni kati ya China na Nigeria. Balozi wa China nchini Nigeria Cui Jianchun anasema,

“Kukamilika kwa ujenzi wa reli ya Lagos-Ibadan na kuanza kwa operesheni zake za kibiashara si kama tu kumeonesha uungaji mkono wa China kwa maendeleo ya uchumi na jamii nchini Nigeria, na bali pia kumeonesha ruwaza ya serikali ya Nigeria. China itaendelea kusukuma mbele ushirikiano wa ‘Ukanda Moja, Njia Moja’ kati yake na Nigeria kwa udhati na uhalisi, chini ya uongozi wa marais wa nchi hizo mbili.”

Bello Sak kutoka Ibadan ni abiria anayetumia usafiri wa treni ya Lagos-Ibadan. Anasema kupanda treni hiyo kunafanana na kupanda ndege.

“Ushirikiano kati ya Nigeria na China ni mzuri sana, na China imefanya kadri iwezavyo, natumai kuwa China itatoa uzoefu mwingi zaidi wa reli kwa Nigeria, kama jinsi inavyotekelezwa vizuri hapa. Tuendelee na juhudi!”