Uhuru Kenyatta: Vikwazo vya upande mmoja vya Umoja wa Ulaya dhidi ya nchi za Afrika havikubaliki
2021-06-24 14:38:33| cri

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ametoa kauli ya kupinga vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya kwa nchi za Afrika na Caribbean bila ya kushauri nchi husika, akionya kuwa maamuzi hayo yanaweza kuharibu ushirikiano.

Akiongea huko Brussels, Ubelgiji, Rais Kenyatta alisema pande zilizoathiriwa zilipaswa kufahamishwa kabla ya kuwekewa vikwazo, na kuongeza kuwa, vikwazo vilivyowekwa dhidi ya nchi za Afrika kama Eritrea na Burundi vimesababisha wasiwasi katika kanda husika.

Rais Kenyatta amesema suala lingine linaloleta wasiwasi ni kuorodheshwa kwenye orodha nyeusi kwa nchi ambazo hazijapitisha sheria za kusimamia au kudhibiti miamala ya kifedha na utakatishaji wa fedha.

Uamuzi uliofikiwa mwezi uliopita uliorodhesha Uganda, Ghana, Zimbabwe na Botswana kati ya nchi za Afrika zinazochukuliwa kuwa zenye "hatari kubwa" kwa mfumo wa kifedha wa Umoja wa Ulaya.