Zanzibar: Makamu wa pili wa Rais azindua sera ya viwanda Zanzibar.
2021-07-20 08:04:05| CRI

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaomba Washirika Binafsi wa Sekta ya Viwanda pamoja na Wadau wa Maendeleo kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa Sera ya Viwanda Nchini ya Mwaka 2019 – 2029 ili ifikie lengo la kuifanya Zanzibar kuwa ya Viwanda. Balozi Seif alitoa ombi hilo wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa Vitabu Vitano vya Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar iliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar. Alisema Sera ya Viwanda ikiwa ni miongoni mwa Vitabu vilivyozinduliwa na kupata baraka zote za Serikali itachangia kuimarika kwa Sekta hiyo kwa kuzingatia utayarishaji wake imewashirikisha wadau wote wa Maendeleo ya Viwanda na kuzingatia maoni na michango iliyotolewa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Sera hiyo ni matokeo ya mapitio ya Sera ya Viwanda ya Mwaka 1998 iliyokuwa imepitwa na wakati ambayo pia inakwenda sambamba na Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 – 2020 ibara ya 84 {d} inayozungumzia kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara. Balozi Seif alisema utekelezaji wa kazi zitaimarisha mazingira bora ya Uwekezaji, uzalishaji wa bidhaa kupitia Viwanda vilivyopo ndani pamoja na kuanzisha vipya ili Taifa lifanikiwe kukabiliana na tatizo la ajira kwa Vijana, kuongeza mapato ya Serikali na kupunguza uagizaji bidhaa kutoka nchi za nje. “Ninatambua kwamba kuitekeleza Sera ya Viwanda ni lazima kila Mshirika apate fursa ya kusoma vitabu hivyo ili aweze kutimize wajibu wake ipasavyo”. Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba kwa vile Sera ya Viwanda Zanzibar imeshapata baraka zote na kukubalika katika ngazi ya juu, hivyo Serikali Kuu itajitahidi kuyatekeleza na kuyasimamia kwa upande wa Sekta ya Umma. Alielezea kuwa vitabu vilivyozinduliwa vinategemewa kuwa na mwanzo mzuri wa kukuza sekta ya Viwanda ambapo Wafanyabiashara watapata uelewa kuhusiana na mazingira ya ufanyaji wa biashara pamoja na kupata muongozo maalum utakaowasaidia wafanyabiashara na bidhaa kupitia daftari maalum. Balozi Seif aliwahakikishia Washirika wa Sekya ya Viwanda na Biashara kwamba Serikali Kuu itazifanyia kazi changamoto zote zilizopo katika urahisishaji biashara katika maeneo ya usafirishaji na uagizaji bidhaa, usajili na uhaulishaji wa mali pamoja na upatikanaji wa vibali.